Imebainika Kuwa Idadi Kubwa ya Watangaza nia ya URAIS 2015 Yaipunguzia Kazi CCM





Imebainika Kuwa Idadi Kubwa ya Watangaza nia ya URAIS 2015 Yaipunguzia Kazi CCM
IDADI kubwa ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuwania nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetajwa kutoa ahueni kubwa kwa vikao vya uamuzi na hasa Kamati Kuu, katika kufanya mchujo wake.

Wakizungumza na gazeti hili kuhusu kuibuka kwa zaidi ya wanachama 30 wa CCM kuwania nafasi hiyo kubwa nchini, wasomi wa fani ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wameelezea namna ambavyo hatua hiyo itakavyorahisisha kazi ya kumpata mgombea.

Mmoja wa wahadhiri wa fani ya siasa chuoni hapo, Dk Jingu John, amesema kujitokeza kwa wagombea wengi, kunatoa fursa nzuri kwa kuwa wangejitokeza wachache, Kamati ya Maadili na Usalama na Kamati Kuu ya CCM ingekuwa katika wakati mgumu kufanya mchujo.

"Katika mazingira ya sasa tunaweza kusema kwa kufuata vigezo na kanuni zao, wanaweza kupata wagombea wazuri kuliko wangejitokeza wagombea kama wawili au watatu, ni kama wamepunguziwa kazi," alisema Dk Jingu.

Msimamo wa JK Mhadhiri mwingine, Dk Benson Bana, alisema msimamo wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete wa kutokuwa na mgombea, umetoa matumaini zaidi ya kutoonesha upendeleo wakati wa kufanya mchujo.

"Chama sasa kinapaswa kudhihirisha kuwa kina uongozi imara, Mwenyekiti anatakiwa ahakikishe kanuni na taratibu zinazingatiwa… kama alivyowahi kusema urais hauna ubia, tunatarajia hata uenyekiti wake hauna ubia," alisema Dk Bana.

Dk Bana alisema hatua ya Kikwete kutokuwa na upande wowote, imeonesha namna alivyokomaa kisiasa ndio maana mpaka sasa hajaonesha upande alioko na hata wagombea wanatarajia haki itatendeka.

Mwanzoni mwa wiki hii Rais Kikwete alipozungumza na Watanzania wanaoishi nchini Uholanzi, alikiri kuwa baadhi ya watangaza nia wamekuwa wakiomba ridhaa yake, ambapo yeye hakuna aliyemkatisha tamaa badala yake amemtakia kila la heri aliyejiona ana ubavu wa kutaka kumrithi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Rais Kikwete katika hilo, alisema ana imani na chama anachokiongoza, kuwa kitafanya chaguo sahihi la mgombea wa urais atakayepeperusha vyema bendera ya CCM katika mchakato wa kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania baadaye mwaka huu.

" Huu ni mwaka wa uchaguzi, kuna mengi yanayoendelea, hasa mchakato wa kuwania urais… huko CCM mpaka leo (Jumatatu iliyopita) watu 15 walishachukua fomu, na wengine zaidi ya 15 ama wametangaza nia au wanakusudia kufanya hivyo.

"Ndiyo demokrasia ndani ya CCM, lakini niwahakikishie acheni waumane, lakini mimi binafsi sina chaguo langu. Chama ndicho kitakachoamua na ninaamini kitatupatia kiongozi sahihi kwa saizi na hadhi ya CCM na huyu atatuvusha mpaka Ikulu. "Jana (Jumapili iliyopita), kuna mtu alinitumia ujumbe akisema anakusudia kutia nia hivyo nimpe baraka zangu…nikamwambia `Good luck' (Kila la heri), sasa kama alitafsiri ndiyo tayari mambo safi, aah…sijui bwana, ila mimi sina mgombea.

"Nasisitiza chama chetu ni makini na kitatupatia mgombea makini. Mwenyezi Mungu atuepushie mbali ili tusipate kiongozi atakayeipeleka nchi pabaya," alisema na kuwataka Watanzania wanaoishi nchini Uholanzi kutokuwa na hofu juu ya mchakato huo ndani ya CCM. CCM kumeguka?

Akizungumzia hofu ya watu kuwa huenda baadhi ya wagombea watakaokatwa wangeweza kutoka katika chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani, Dk Bana alisema haoni mgombea hata mmoja aliyejitayarisha kuhamia upinzani na ikitokea, haoni namna mgombea huyo atakavyojijenga kisiasa.

Vikao vya mchujo Mchakato wa uchukuaji fomu za kuomba ridhaa ya CCM kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Zanzibar ulioanza Juni 3 mwaka huu, unatarajiwa kukamilika Julai 2 mwaka huu.

Baada ya kuchukua fomu, kila mgombea ametakiwa kuzunguka mikoa 15 nchi nzima, mitatu lazima iwe ya Zanzibar kusaka wadhamini 450, wastani wa wadhamini wasiopungua 30 kila mkoa, hatua ambayo imekuwa ikiendelea na kugonganisha wagombea katika mikoa mbalimbali nchini.

Kwa upande wa nafasi ya urais wa Zanzibar, ambayo mpaka jana hakukuwa na mgombea hata mmoja aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo, mwanachama atakayechukua fomu, atatakiwa kutafuta wadhamini 250 kutoka mikoa mitatu ya Unguja na Pemba.

Baada ya kazi ya kupata wadhamini kukamilika, vikao mbalimbali vya uchujaji wa majina ya wagombea vinatarajiwa kuanza, vikitanguliwa na kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili, kitakachokutana Julai 8, mwaka huu.

Kikao hicho kinatarajiwa kuandaa mapendekezo, yatakayosomwa na kujadiliwa na kikao cha Kamati Kuu kitakachokutana Julai 9, ambacho ndicho kinachoelezewa na wasomi kuwa kitakuwa na kazi nyepesi ya kuchuja majina ya wagombea, ili wapatikane wasiozidi watano watakaopelekwa kwa mchujo zaidi katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.

Kikao cha Nec kinachotarajiwa kukutana Julai 10 mwaka huu, kitachuja majina hayo zaidi na kutoka na majina matatu, yatakayopelekwa katika Mkutano Mkuu utakaofanyika kwa siku mbili za Julai 12 na Julai 13 mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo ndio utakayemtoa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa CCM na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho.

Wagombea Wanachama na vigogo waliokwisha kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo kubwa kitaifa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mkazi wa Musoma mkoani Mara, Boniface Ndengo, mkulima kutoka kijiji cha Mjimtala wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Eldefonce Bilohe na kada wa siku nyingi wa chama hicho, Dk Hassy Kitine.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimri), Dk Mwele Malecela na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kingwangalla.

Pia yupo Balozi Amina Salum Ally, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wassira, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.

Wengine ni Balozi Ally Karume, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, Mtumishi wa CCM Idara ya Siasa na Uhusiano wa Tanzania, Amos Siyantemi na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.

Pia yupo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Wakili Mwandamizi Mahakama Kuu Tanzania, Godwin Mwapango, na makada wengine wa CCM, Peter Nyalile na Leonce Mulenda.

Wengine aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, Balozi Agustino Mahiga, Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Monica Mbega na kada wa CCM kutoka mkoani Tanga, Dk Mzamini Kalokola.

Comments