Hotuba ya KUB, Freeman Mbowe bungeni - Mei 12, 2015

Hotuba ya KUB Freeman Mbowe bungeni leo


*HOTUBA YA KIONGOZI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE.FREEMAN AIKAELI
MBOWE (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA
KATIKA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016*
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99 (9), ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la
Mwaka 2013)
______________________________ ___

*1. **UTANGULIZI:*

*Mheshimiwa Spika,*
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na
kunitunza ili niweze kutumikia taifa langu. Napenda kuishukuru familia
yangu kwa msaada mkubwa na uvumilivu hasa katika harakati na shughuli zangu
za kisiasa.

*Mheshimiwa Spika,*Napenda kuchukua nafasi hii pia, kuwashukuru watanzania
wote kwa ujumla kwa kupokea na kulea harakati za mabadiliko nchini.
Shukrani hizi za pekee ziwafikie wenyeviti wenza wa vyama vinavyounda UKAWA
, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba, Mhe. James Mbatia na Mhe. Dk Emanuel Makaidi.
Vilevile, kwa makatibu wakuu viongozi wa UKAWA Mhe. Maalimu Seif Shariff
Hamad, Mhe. Wilbroad Slaa, Mhe. Mosena Nyambabe na Mhe. Tozi Matwange.
Aidha, shukrani hizi ziende kwa timu ya wataalamu wa UKAWA, viongozi,
watendaji, wanachama na wapenzi wa vyama vyetu vinavyounda UKAWA vya NLD,
CUF, NCCR-Mageuzi na CHADEMA. Niwatake wanachama na wapenzi wa UKAWA
kujipanga, kujituma na kujiandaa kushinda kwa kishindo na kushika dola
katika Uchaguzi Mkuu wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, shukrani za pekee ziende kwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani
Bungeni wanaounda UKAWA kwa kazi nzuri ya kutetea na kusimamia maslahi ya
wananchi. Na pia kwa watendaji wa Kambi ya Upinzani ambao wamekua msaada
mkubwa kwetu na kwa kazi yao nzuri kwa taifa letu.

*Mheshimiwa Spika,*Napenda kuwashukuru kwa kipekee, wananchi wa Jimbo letu
la Hai kwa ushirikiano mkubwa na imani waliyonayo kwangu kama mwakilishi
wao. Niliwaahidi kuwatumikia kwa moyo wangu wangu wote na naendelea
kuwaahidi kuwa imani yao kwangu haitopotea bure.

*Mheshimiwa Spika,*Napenda kuwashukuru kwa kipekee wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Peter Kayanza
Pinda, Spika wa Bunge Mhe. Anna Makinda, Naibu Spika Job Ndugai na Katibu
wa Bunge Ndugu Dk. Thomas Kashilila pamoja na wafanyakazi wa Bunge kwa
ushirikiano mliotupa toka kuanza kwa Bunge la 10, vilevile napenda
kuwatakia heri Mhe. Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mhe. Spika Anne Makinda
katika maisha mengine nje ya siasa za Bunge kwani walishatangaza kustaafu
ubunge.

*Mheshimiwa Spika,*Baada ya shukrani hizo za kipekee napenda kunukuu maneno
machache kutoka kwa Nelson Mandela aliyepata kusema; *"I learned that
courage was not the absence of fear, but the triumph over it. The brave man
is not he who does not feel afraid, but he who conquers that fear."
*"Nimejifunza
kwamba ujasiri si kukosekana wa uoga bali ushindi dhidi ya uoga. Mwanadamu
jasiri si Yule ambaye hahisi uoga bali Yule anayeshinda uoga" Vilevile
Nelson Mandela alipata kusema; *"When a man is denied the right to live the
life he believes in, he has no choice but to become an outlaw." *"Pale
Binadamu anaponyimwa kuishi maisha anayoyaamini, huwa hana njia bali kuwa
mvunjaji wa Sheria"

*2. **MWAKA WA TUMAINI JIPYA* *Mheshimiwa Spika,* Huu ni mwaka ambao nchi
yetu itafanya uchaguzi Mkuu wa Kihistoria ambao utakitoa chama ambacho
kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 50 na hivyo kujikuta kimechoka na
kukosa mawazo mapya na ya kisasa ya kuendesha na kuendeleza nchi yetu.
Ukweli huu mchungu ni vyema ukaanza kuwaandaa kisaikolojia wote walioko
kwenye mamlaka kutambua kwamba kubadilisha chama kinachoongoza Taifa siyo
jambo geni duniani. Ni fursa ya nchi kutafuta muelekeo mpya wenye kujaza
tumaini jipya, fikra mbadala na SHAUKU ya kuondokana na uendeshaji wa
kimazoea wa Serikali na maisha ya wananchi wake. Nipende kuwahakikishia
wote, hususan walioko madarakani kuwa UKAWA umedhamiria kwa dhati kurejesha
utawala bora wenye kuzingatia haki na sheria, usimamizi makini wa
rasilimali na tunu za Taifa na umekusudia kujenga Tanzania mpya yenye
mshikamano wa kweli, uhuru wa kweli, amani ya kweli na ustawi wa wote bila
kubagua kwa misingi ya kiitikadi, dini, kabila, jinsia au rangi kama ilivyo
leo.

*Mheshimiwa Spika,* Kutokana na umuhimu wa mwaka huu kuwa wa uchaguzi Mkuu
kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu nitajikita zaidi kwenye eneo hilo. Lengo
ni kuweka rekodi sahihi kuwa sisi Kambi ya Upinzani tulionya sana na kwa
muda mrefu kuhusu umuhimu wa uwazi na maandalizi shirikishi ya mapema ili
kulihakikishia taifa mserereko salama wa mpito, yaani "smooth transition"
kutoka awamu ya nne ya Utawala wa nchi yetu kwenda awamu ya tano. Mpito
salama ambao utatokana na kuwepo kwa uchaguzi huru, wa haki na uwazi.

*3. **DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA (BVR)*

*Mheshimiwa Spika, *Tume Taifa ya Uchaguzi imeanza zoezi la kuandikisha
upya wapiga kura katika mfumo mpya wa kielectronic ambao unajulikana kama
BVR na zoezi hili lilianzia katika mji wa Makambako mkoani Njombe Mwezi
Februari 2015 na Sasa linaendelea kwenye baadhi ya Kata za Mikoa ya Lindi,
Mtwara, Ruvuma, Iringa na Mbeya .

*3.1 Hujuma za Serikali dhidi ya Tume :*

*Mheshimiwa Spika ,* Pamoja na kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu ilijulikana
tangu tulipomaliza uchaguzi mkuu uliopita, Serikali ama kwa makusudi ama
kwa kugubikwa na misukumo ya kimaslahi, imeshindwa kukamilisha daftari la
kudumu la wapiga kura kwa wakati muafaka. Pamoja na mengine, Ucheleweshaji
wa kuandikisha wapiga kura umesababishwa na Tume kutopewa fedha na Serikali
kwa wakati muafaka. Mwezi Februari 2013 wakati Rais Kikwete akizindua
vitambulisho vya taifa alisema vitambulisho hivyo ndivyo vitakavyotumiwa
katika kura ya maoni na uchaguzi mkuu. Hata hivyo Serikali haikufanya
uratibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Tume ya Uchaguzi ili
taasisi mbili zishirikiane na kukamilisha zoezi hili. NIDA haikupewa fedha
za kutosha kukamilisha zoezi la kuandikisha na kutoa vitambulisho vya
taifa. Tume ya Uchaguzi ikaanzisha mchakato wa kuandikisha wapiga kura bila
kutengewa fedha za kutosha za kununulia vifaa, kuajiri na kuwapa mafunzo
wafanyakazi husika, na kutoa elimu kuhusu kujiandikisha kwa wananchi.

*Mheshimiwa Spika,* Hivi sasa serikali inaonekana kuwa na matatizo makubwa
ya fedha baada ya wahisani kusitisha kutoa fedha za msaada wa bajeti kwa
sababu ya ufisadi wa kutisha wa Tegeta Escrow Account.

*Mheshimiwa Spika, **Pamoja na ukweli kuwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi
inahitaji Tume kuboresha*Daftari la Kudumu la Wapiga kura angalau mara
mbili kati ya uchaguzi mkuu na unaofuata; Kwa makusudi Serikali iliamua
kuivunja sheria ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura. *Kambi rasmi
ya Upinzani Bungeni* inaona kuwa ,Kitendo hiki kina malengo na nia mbaya ya
kutaka kuongezea muda wa utawala wa Rais Kikwete kwa kisingizio kuwa
uchaguzi mkuu hauwezi kufanyika kwani daftari la kudumu la wapiga kura bado
halijakamilika kuboreshwa.

*3.2 Udhaifu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika BVR.*

*Mheshimiwa Spika , *Pamoja na zoezi kuanza kwa kusuasua ni wazi kuwa Tume
haina watumishi wa kufanya kazi katika zoezi hili muhimu kwa uhai wa Taifa
* , *pamoja na ushauri wa mshauri Mwelekezi kutoka Kampuni ya *IPSITI* ya
Nchini Marekani na ambayo ripoti iliwasilishwa kwa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi mwezi Januari 2015 , Mshauri ambaye Tume ilimpa majukumu ya
kuwashauri na kumlipa mamilioni ya fedha za walipa kodi na hata
alipowashauri Tume kuwa wanahitaji kuwa na zaidi ya watumishi 10,000 kwa
ajili ya kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaweza kufanyika kwa ufanisi na
kufanikiwa kwa nchi nzima. Mshauri huyo mwelekezi alienda mbele zaidi na
kuwaambia Tume kuwa Ni lazima watumishi hao wawe wamepatiwa mafunzo ya kina
kuhusu jinsi ya kuweza kutumia mfumo huu mpya wa BVR kuandikisha wapiga
kura na hata jinsi ya kutumia mashine zenyewe .

*Mheshimiwa Spika, *Jambo la kusikitisha ni kwamba Watumishi wa Tume ambao
wameanza kufanya kazi ya kuandikisha wapiga kura wamepatiwa mafunzo kwa
muda wa siku moja au mbili tu kabla ya zoezi la kuandikisha wapiga kura
kuweza kuanza , kati yao wapo watanzania ambao wamepewa kazi hiyo na
hawajawahi kutumia Kompyuta kabisa katika maisha yao na hata hizi mashine
ni mara ya kwanza kuonekana na kutumika Nchini mwetu, na hivyo kulifanya
zoezi kuwa gumu zaidi kutokana na watumishi kutokupata mafunzo ya kutosha
na hivyo kuweza kuwasaidia katika kutumia mashine za BRV na hata wanapoanza
kupata uzoefu muda wa kuandikisha unakuwa umeisha ,yaani siku saba. Aidha ,
baadhi ya Wapiga picha wameshindwa kutimiza majukumu yao kwa wakati kwani
wanashindwa kutumia Kamera ambayo wamepewa kwa ufanisi na hivyo kulifanya
zoezi kwenda taratibu sana na foleni kuwa ndefu vituoni.

*Mheshimiwa Spika, *Tume haisemi kweli kuhusiana na zoezi hili. Mara
kadhaa, viongozi wa Tume wamekuwa wakitoa kauli kadhaa zisizotekelezeka na
kisha kuzibadilisha bila maelezo yenye mantiki. Tume imeendelea kusisitiza
kuwa zoezi hili litaweza kukamilika kwa muda uliopangwa bila kuweka
hadharani imani hiyo inatokana na nini ilhali mazingira yote ya kisayansi
yanaonyesha kinyume. Ikiwa Tume ina nia ya kuwapa fursa ya kujiandikisha
Watanzania wote takribani milioni 24 wenye sifa na haki ya kupiga kura,
haiwezekani ikakamilisha mchakato mzima kabla ya kuanza kwa kampeni mwezi
wa Agosti 2015 labda pengine miujiza ifanyike.

*Mheshimiwa Spika, *Tume haitaweza kuandikisha wapiga kura wote kwa muda wa
siku saba ambazo imeweka kwa kila kituo .— Kwa mujibu wa taarifa ya
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Lubuva alipokuwa anamkaribisha
Waziri Mkuu Pinda kuzindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura katika Mji wa
Makambako alisema kuwa tarehe 24 /2/2015 waliweza kuandikisha wapiga kura
3,014 katika vituo 55. Yaani kila mashine moja ilikuwa na uwezo wa
kuandikisha wastani wa wapiga kura 54 kwa siku, hii maana yake ni kuwa kama
tume ikiweza kupata mashine zote 7750 ilizoagiza kwa wakati na kuwa na
jumla ya mashine 8000 inaweza kuandikisha wapiga kura 432,000 kwa siku na
hivyo kwa siku 7 za ratiba ya tume kwa kutumia mashine zote 8000 wataweza
kuandikisha wapiga kura 3,024,000 tu.

*Mheshimiwa Spika ,* Ili kuandikisha wapiga Kura 24,000,000 wanaokisiwa,
itahitajika wastani wa siku 56 kila mashine kuandikisha kwenye vituo nchi
nzima ili kukamilisha zoezi hilo na bila mashine kuharibika. Na hivyo ni
ukweli uliowazi kuwa mpaka tarehe ya mwisho ambayo haijajulikana kwani Tume
haijasema itaandikisha wapiga kura mpaka lini ili kuwe na muda wa kuhakiki
Daftari lenyewe , kwa mwendo huu wa kuandikisha wapiga kura 54 kwa mashine
moja kwa siku, lengo la kuandikisha wapiga kura wote 24 milioni
halitawezekana kwa muda huu ambao Tume imelitangazia taifa.

*Mheshimiwa Spika, *Zoezi hili linaendelea kufanyika licha ya Tume kutokuwa
na vifaa vya kutosha kama ambavyo iliomba ipatiwe na serikali BVR kits
10,500 lakini serikali ikawaahidi kuwapatia KITS 8000 na ambazo mpaka leo
hazijafika nchini zote kwa kuwa serikali ilichelewesha fedha makusudi na
hivyo Mkandarasi akasimamisha uzalishaji wa mashine hizo hadi Serikali
ilipomalizia malipo hayo mwezi Machi mwaka huu na hii ni kwa mujibu wa
Randama ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo wamesema , nanukuu uk.10* 'Baada
ya kupatikana fedha kidogo kwa ajili ya uendeshaji, zoezi la Uboreshaji
limeanza tarehe 23 Februari,2015 katika Mkoa wa Njombe , Halmashauri ya Mji
wa Makambako na baadaye mikoa mingine itafuata kulingana na kufika kwa BVR
Kits 7,750 zilizobaki.'*Mwisho wa kunukuu. Hii ni taarifa ya tume ya April
,2015.

*Mheshimiwa Spika , *Tume kwenye randama yao wameendelea kueleza kuwa ,
nanukuu uk.10 '*Awali Tume ilipanga kutumia BVR kits zipatazo 10,500 kwa
nchi nzima,lakini baadaye zilipunguzwa hadi BVR kits 8,000 baada ya
majadiliano na Serikali'* Hii maana yake ni kuwa Serikali iliamua makusudi
kupunguza BVR kits hizo bila kujali ushauri wa kitaalamu wa Tume. Na hata
baada ya kupunguza mashine hizo bado ilishindwa kuzilipia kwa wakati ili
kuiwezesha tume kuandikisha wapiga kura kwa mujibu wa kalenda yao jambo
ambalo sasa linatishia uhakika wa kuwepo kwa uchaguzi Mkuu hapo Mwezi
Octoba.

*Mheshimiwa Spika, *Tume haijatoa taarifa za kutosha kwa wadau wote kuhusu
teknolojia ya BVR, kampuni inayotengeneza mashine zinazotumiwa, kampuni
gani iliyopewa tenda ya programu ya kompyuta (software) itakayoendesha na
kusimamia daftari la kudumu, taratibu za kuhifadhi kumbukumbu, usafirishaji
wa kumbukumbu kutoka vituo vya kuandikisha wapiga kura, mashine za kutambua
wapiga kura siku ya uchaguzi na kadhalika.

*Mheshimiwa Spika,* Kutokana na tume kukosa mashine hizo imeamua kupunguza
siku za kuandikisha wapiga kura kutoka 14 za awali na sasa wanaandikisha
kwa siku 7 tu kwa kituo jambo ambalo limeanza kuwa na madhara kwani wapiga
kura wengi wanaachwa bila kuandikishwa. Mfano mzuri ni Wilayani Namtumbo
ambako mkandarasi aliyepewa jukumu la kubeba vifaa alihamisha bila kujali
kuwa kuna wananchi ambao walikuwa kwenye misururu ya foleni vituoni humo.

*Mheshimiwa Spika, *Tume pia haijatoa taarifa juu ya vituo vya kuandikishia
wapiga kura na idadi ya wapiga kura inayotegemea kuandikisha kila kata.
Katika zoezi la majaribio la uandikishaji wapiga kura katika Jimbo la Kawe
wilaya ya Kinondoni, Tume iliandikisha wapigakura katika kata ya Bunju na
Mbweni. Katika kata hizo Tume iliandikisha wapigakura 15,123 na kuvuka
lengo iliyojiwekea la wapiga kura 14,312 kwa karibu asilimia 6. Hata hivyo
matokeo ya Takwimu za Sensa ya watu ya mwaka 2012 yanaonesha kuwa kata ya
Bunju ina wakazi wenye sifa za kuwa wapiga kura 42,227 na Mbweni wapigakura
9,650. Idadi hii haijajumlisha watu waliohamia maeneo hayo baada ya sensa.
Walioandikishwa katika kata mbili za Kawe ni chini ya asilimia 30 ya
wapigakura wanaostahiki kuandikishwa.

*Mheshimiwa Spika, *Siku 7 hazitoshi kuandikisha wapiga kura wote kwa kila
kata, na hasa ikizingatiwa kuwa Tume inaandikisha wapiga kura msimu wa
masika wakati wananchi wengi wako katika shughuli za kilimo na vituo viko
nje hivyo kuathiri utendaji kazi. Kwa hiyo muda wa ziada unahitajika
kuwaandikisha. Matatizo yanayojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapiga
kura yanaonesha wazi kuwa daftari la wapiga kura halitakamilika ili
litumiwe katika zoezi la Uchaguzi Mkuu. Ni vyema Waziri Mkuu na Serikali
mkakubali ukweli huu kuwa bila mkakati wa makusudi wa kuiwezesha na
kuisimamia Tume ya Taifa ya Uchaguzi , hakuna uchaguzi Octoba.

*Mheshimiwa Spika,* Kama kuna jambo litawasha nchi hii ni mkakati wowote wa
kujaribu kuongeza muda wa kuwepo madarakani Serikali ya awamu ya nne.
Chaguzi kwa mujibu wa Katiba siyo jambo la kuchezea hata kidogo. Tume na
Serikali zimekuwa zikitoa majibu mepesi tena wakati mwingine ya kejeli kwa
maswali magumu. Ni dhahiri, tume imetumika kama "mshirika na msiri" wa
Serikali. Tume inajua uchafu na ufisadi mwingi unaogubika uagizaji na
uingizaji wa BVR kits lakini imeendelea kudumisha siri hii. Kuhairisha
uchaguzi kwa uzembe wa aina hii haikubaliki. Ni vyema Bunge lako likajadili
kwa kina ratiba ya uchaguzi mwaka huu na wote waliozembea na kulisababishia
Taifa hofu ya kiwango hiki wawajibishwe haraka. Aidha, tume nzima ya
uchaguzi ijitafakari kama kweli ina weledi wa kuendelea kuwepo na kusimamia
uchaguzi mkuu ujao bila kusababisha machafuko makubwa nchini,

*Mheshimiwa Spika, **Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni* ,Tulisema kuwa kura
ya maoni haitawezekana kufanyika tarehe 30 mwezi Aprili , lakini serikali
na tume hii hii iliendelea kutubeza. Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na hata
Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi waliendelea kusisitiza kuwa kura ya maoni ya
Katiba pendekezwa itafanyika. Tarehe 30 Aprili kura ya maoni haikufanyika
na haijulikani hatma yake. Fedha za walipa kodi zimepotea kwa mabilioni.
Hakuna aliyewajibika.... huo ndiyo utawala wa Rais Kikwete. Hii ndiyo CCM.

*Mheshimiwa Spika, *Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupata majibu
kutoka serikali hii ya CCM kwenye mambo yafuatayo; i. Mashine za BVR
zitawasili lini nchini kwa ukamilifu wake? ii. Tume itamaliza lini (tarehe)
kuwaandikisha Watanzania wote wenye sifa ya kuwa wapiga kura katika Daftari
la wapiga kura? iii. Ni lini Watanzania ambao watakuwa wameandikishwa
kwenye Daftari la wapiga kura watapata fursa ya kuhakiki Daftari la wapiga
kura kwa mujibu wa sharia na zoezi hili litachukua muda gani? iv. Je, Tume
itaweza kufanya maandalizi mengine ya kina ya uchaguzi Mkuu na ikizingatiwa
kuwa muda wote itakuwa inaendelea kuandikisha wapiga kura? v. Tume itaweka
lini hadharani mpango mzima na ratiba za utekelezaji kuelekea uchaguzi mkuu
wa tarehe 25 Octoba 2015 ambapo kwa mujibu wa sharia zimebaki siku pungufu
ya 100 kwa kampeni za uchaguzi kuanza.

*3.3 Mpango haramu wa Tume: Watanzania 2.9 milioni kutokuandikishwa:*

*Mheshimiwa Spika, *Kutokana na kukosekana kwa muda na vifaa vya kutosha
kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura wote wenye sifa kwa mfumo wa BVR ,
Tume imeshaamua kwa makusudi kutokuwaandikisha wapiga kura zaidi ya *milioni
2.9* katika zoezi linaloendelea. Hii ni kwa mujibu wa taarifa rasmi za Tume
ya Taifa ya Uchaguzi iliyoko kwenye Randama yake. Nanukuu uk.10* 'Tume ya
Taifa ya Uchaguzi inakadiria kuandikisha wapiga kura 21 milioni kati ya
watanzania 23.9 milioni wenye sifa za kuwa wapiga kura, kulingana na
Takwimu za Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2012. Makisio ya wapiga kura
inazingatia wale ambao hawatajiandikisha kutokana na Voter Apathy'*

*Mheshimiwa Spika, *Tafsiri ya kuwaacha bila kuwaandikisha Watanzania *2.9
Milioni *kama Tume inavyosema kwenye randama yake kwa hoja ya*'Voter
Apathy'*, maana yake ni sawa na kuacha mikoa zaidi ya sita ya Tanganyika
bila kumwandikisha mwananchi hata mmoja. Mikoa hiyo (kwenye mabano ni
takwimu za wenye sifa za kuandikishwa kwa mujibu wa sensa ya 2012)
Lindi *(0.518
milioni),* Singida *(0.698 milioni),* Njombe *(0.392 milioni),* Katavi *(0.271
milioni), *Rukwa *(0.472 milioni)* na Iringa *(0.524 milioni).*

*Mheshimiwa Spika,* Tume inataka kuhalalisha kuacha kuandikisha Watanzania
wengi kiasi hicho kwa hoja dhaifu kama hiyo? Kazi ya Tume ni kuwaandikisha
Watanzania wote wenye sifa na hivyo basi Tume inatakiwa kuhakikisha kuwa
inatoa *elimu kwa umma, hamasa na umuhimu wa kujiandikisha* katika Daftari
la Kudumu la wapiga kura kwa Watanzania na sio kukaa kimya bila kufanya
matangazo ya kina ya kuwahamasisha wananchi kama wanavyofanya sasa na
kuishia kujificha kwenye kichaka cha *'Voter Apathy'* hali hii haikubaliki
hata kidogo.*Kambi Rasmi ya Upinzani*, tunataka kujua kutoka serikalini
Tume imetumia kigezo gani cha kusema kuwa zaidi ya asilimia 12.1 ya
Watanzania wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura
hawatajiandikisha mwaka huu? Imefanya utafiti huo lini, na ripoti yake iko
wapi? Au huu ni mkakati wa makusudi ambao unaoratibiwa na serikali ya CCM
na Tume wa kupunguza wapiga kura baada ya Tume kutokupewa vifaa vya kutosha
kwa ajili ya kuwaandikisha watu wote wenye sifa? Ama huu ndio mpango mzima
wa hujuma ambao unaendana sambamba na kupunguza muda wa kuwaandikisha
wapiga kura kutoka siku 14 kama ilivyokuwa imepangwa awali na kuwa siku 7
za sasa ? *Aidha, *tunaitaka serikali kutoa majibu ya kina imejipanga vipi
katika kuwahamasisha, kuwaelimisha na hatimaye kuwaandikisha kwenye Daftari
la Kudumu la Wapiga kura Watanzania wote wenye sifa za kuandikishwa kwa
muda wa siku saba ambazo tume imeweka kwa kila kituo?

*3.4 Takwimu za Tume ni Utata Mtupu:*

*Mheshimiwa Spika,* Kwa Mujibu wa Takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni
kuwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 Watanzania waliojiandikisha kupiga kura
walikuwa *16.4 Milioni* na waliojitokeza kupiga kura walikuwa *11.3
milioni,* Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 walijiandikisha watanzania*20.1
Milioni* na waliopiga kura walikuwa *8.3 Milioni .* *Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni,* inataka majibu ya swali hili, Tume inaposema kuwa Mwaka
2015 itaandikisha wapiga kura *21 Milioni ,* maana yake ni kuwa tangu mwaka
2009 ambapo ndio ilikuwa mara ya mwisho kuandikisha wapiga kura, watanzania
ambao umri wao umeongezeka na hivyo kuwa na sifa za kuandikishwa kwenye
Daftari ni *0.9* *Milioni* tu au kuna mchezo mchafu ambao umepangwa
kuchezwa na Tume ikishirikiana na Serikali ya CCM? Ama serikali na Tume
inataka kusema kuwa tangu 2009 Watanzania ambao walikuwa wamejiandikisha
wamefariki dunia na hivyo kufanya idadi ya watu wenye za kujiandikisha kuwa
kiasi hicho?

*4. **MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU ,2015.*

*4.1 Tume haijapewa fedha kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi Mkuu.*

*Mheshimiwa Spika, *Pamoja na ukweli kuwa muda haupo upande wetu lakini
mpaka sasa hakuna maandalizi yoyote ambayo yamefanyika na yenye kuashiria
kuwa uchaguzi mkuu unaweza kufanyika mwezi Octoba,2015 kwa mujibu wa Katiba
.Ukweli huu umethibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwenye randama yao
walipoandika, nanukuu uk.13 *'Kwa upande wa Maandalizi ya Kura ya Maoni na
Uchaguzi Mkuu,2015 Tume hatujapokea fedha hadi sasa'*

*Mheshimiwa Spika*, *Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,* inajiuliza Kama
serikali haijaipatia Tume fedha kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu,
wanategemea miujiza gani kuwa ifikapo Octoba uchaguzi Mkuu utafanyika? Ni
lini Zabuni zitatangazwa kwa ajili ya wakandarasi mbalimbali ambao
watasambaza vifaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, na tarehe ya kuwapata hao
wazabuni ni lini ?

*Mheshimiwa Spika, *Wakati Serikali hii ikishindwa kuipatia fedha Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu Octoba,
2015 ili uweze kufanyika katika mazingira ya amani, haki na utulivu,
Serikali hii ya CCM imeamua kuwekeza na kujiandaa kupambana na wananchi
wake, hii ni kutokana na ukweli kuwa ,wakati Tume inakosa fedha za kulipia
vifaa kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura na kufanya maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu , tuna taarifa kuwa Serikali imeamua kuagiza zaidi ya *magari
777* kwa ajili ya Jeshi la Polisi, kuanzia yale ya Maji ya kuwasha, Doria
na shughuli za Ukaguzi katika Mwaka huu wa Fedha.

*Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni , *inajiuliza kwamba hivi ni nini
kipaumbele chetu kama taifa kwa sasa? Je, ni kuandaa mazingira ya kufanyika
kwa uchaguzi mkuu kwa hali ya haki, amani na utulivu? Au ni kujiandaa
kuuvuruga uchaguzi huo? Ndiyo maana tunashuhudia jitihada hizi za kujiandaa
kupambana na wananchi wakati uchaguzi Mkuu utakaposhindikana kufanyika kwa
sababu ya kukosekana kwa maandalizi thabiti na ya kina ya kuwezesha
kufanyika kwa uchaguzi huo? Na hizo ndio sababu za serikali hii ya CCM
kukataa kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na kuwekeza
katika Mapambano?

*4.2 Aibu ya Tume na Madeni :*

*Mheshimiwa Spika, *Pamoja na Tume ya Uchaguzi kutokupewa fedha kwa ajili
ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na Serikali hii ya CCM , bado Tume wanadaiwa
madeni na wakandarasi ambao walisambaza vifaa kwa tume kwenye Chaguzi
mbalimbali zilizopita, madeni hayo ya Tume yanathibitishwa na maandishi ya
Tume kwenye randama yao uk .13 nanukuu *'Hata hivyo kuna Wazabuni waliotoa
huduma ambao wanatudai fedha kiasi cha USD 8,377,134.56.....'* Hizi ni sawa
na *Shilingi Bilioni 16.754* kwa viwango vya bei ya soko leo kutokana na
kudorora kwa shilingi, laiti kama deni hilo lingeweza kulipwa mapema kabla
ya Shilingi kudorora na kuporomoka tusingekuwa na deni kubwa kiasi hiki leo
hii. Aidha kutokana na Tume kudaiwa kiasi hicho cha fedha wakandarasi
wameshindwa kuiamini tume na ndio maana haikopesheki tena na hivyo
kushindwa hata kuanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu Octoba 2015, kwa njia ya
Mkopo,hawana pa kukopa!

*Mheshimiwa Spika,* Ukiangalia* Jedwali Na:4 Makadirio ya Matumizi ya
Kawaida kwa Mwaka 2015/16* kwenye randama ya Tume utaona kuwa fedha
iliyoombwa ni kiasi cha shilingi *192.409 Bilioni,* na fedha hizo zimeombwa
kwa ajili ya Mishahara *2.144 bilioni,* Matumizi mengineyo *2.302 bilioni* na
kiasi cha *shilingi 187.962 bilioni* kwa ajili ya uendeshaji wa Uchaguzi
Mkuu.*Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,* inauliza hivi deni la zaidi ya *bilioni
16* ambazo tume inadaiwa na wakandarasi hazitalipwa mwaka huu wa Fedha? Na
kama zitalipwa zitatoka fungu gani hasa ikizingatiwa kuwa tayari Tume
imeshatoa rai kuwa fedha zake ziwekwe kwenye *Fungu 61* na sio Mfuko Mkuu
wa Hazina ambao ulikuwa ukitumika kama kichaka cha kuficha ukweli katika
bajeti zilizopita.

*4.3 Fedha za Uendeshaji Uchaguzi Mkuu hazina Mchanganuo:*

*Mheshimiwa Spika,* Tume ya Taifa ya uchaguzi wameomba kupatiwa kiasi cha
shilingi *187.962 Bilioni* kwa ajili ya uendeshaji wa Uchaguzi ambao
unapaswa kufanyika Octoba ,2015 kwa mujibu wa Katiba yetu, fedha hizi
hazina maelezo wala mchanganuo wake kuwa zinaombwa kwa ajili ya kulipia
kitu gani hasa , ni Mawakala ,vifaa vya uchaguzi au ni kwa ajili ya kulipia
posho kwa wasimamizi wa uchaguzi huo?

*Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni* inataka kupatiwa mchanganuo wa *kasma
229914* :Uendeshaji wa Uchaguzi Mkuu kiasi cha*sh.187,962,160,000* hizi ni
fedha kwa ajili ya vitu gani na hasa ikizingatiwa kuwa Tume haijatangaza
zabuni kwa ajili ya vifaa vya Uchaguzi Mkuu, wamekokotoa kiwango hicho
kutokana na msingi upi? Au wamefanya mazoea ? wamezingatia kiwango cha
kuporomoka kwa shilingi na hasa kwa vifaa ambavyo tutalazimika kuagiza
kutoka nje ya Nchi ?

*Mheshimiwa Spika*, Kwa mujibu wa randama ya Tume imeonyesha kuwa Tume
tayari imeshafanyia maboresho sheria na kanuni za uchaguzi, na hiyo ipo uk
12 wa randama , naomba kunukuu .*..'imeanza pia kufanya Maboresho ya Sheria
na Kanuni za Uchaguzi...' *Kambi rasmi ya Upinzani inataka kujua ni lini
sheria hizo zitawasilishwa Bungeni? kwani kwa mujibu wa Katiba chombo
chenye mamlaka ya Kuboresha ama kubadilisha sheria ni Bunge na sio chombo
kingine chochote kile , na hasa ikizingatiwa kuwa hili ni Bunge la Bajeti
na la mwisho kabla ya uchaguzi Mkuu Octoba 2015. Maboresho hayo ya sheria
yatafanyika wapi na kupitishwa lini ?

*Mheshimiwa Spika,* Tume pia imeonyesha kwenye randama yake kuwa kuna
mpango wa kupitia upya mipaka na majina ya majimbo ya Uchaguzi , nanukuu
randama uk.12 *.....'kupitia mipaka na majina ya Majimbo ya Uchaguzi na
kuyarekebisha ....'* Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu
ni majimbo yapi ambayo yatahusika na mpango huu wa Tume na hasa
ikizingatiwa kuwa tayari vyama vimeshaanza michakato yake ya ndani ya
kutafuta na kuteua wagombea wa nafasi za Udiwani, Ubunge,Uwakilishi na
Urais. Ni vyema Tume ikayatangaza mapema Majimbo hayo ili wananchi pamoja
na wadau wa uchaguzi (Vyama vya siasa) wakapata muda wa kutosha wa
kujiandaa na hasa kuandaa wagombea katika Majimbo hayo.*Kambi rasmi ya
Upinzani* , inakubaliana na rai ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama ilivyo
kwenye randama yake uk.14 nanukuu *'Fedha kwa ajili ya shughuli za Uchaguzi
ziwekwe kwenye Fungu 61 badala ya kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, ili
kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kulingana na Ratiba' *Kwani ni
ukweli uliowazi kuwa Mfuko Mkuu wa Hazina umekuwa kama kichaka cha kuficha
mambo na hasa ikizingatiwa kuwa hata bajeti ya mwaka 2014/2015 Kambi rasmi
ya Upinzani tulipohoji ziko wapi fedha za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu
tuliambiwa kuwa ziko Mfuko Mkuu wa Hazina jambo ambalo halikuwa kweli na
ndio maana Tume haijapewa hata senti moja kwa ajili ya Maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu wa octoba 2015 . Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , inaitaka
serikali kufuata ushauri wa Tume ya Uchaguzi wa kuhakikisha kuwa haiongezi
maeneo ya utawala tunapokaribia Uchaguzi kwani kunaifanya Tume kushindwa
kupanga mipango yake katika kuandaa uchaguzi Mkuu .

*5. **KURA YA MAONI *

*5.1Kura ya maoni haipo kwa mujibu wa sheria ;*

*Mheshimiwa Spika , *Pamoja na utamaduni wa Serikali hii wa kuvunja sheria
zilizotungwa na Bunge lako kuwa ni jambo la kawaida , tumeshuhudia kuvunjwa
kwa sheria ya kura ya maoni kwa kiwango ambacho hakivumiliki tena .Hali
hiyo imeipelekea hata Tume ya Uchaguzi kushindwa kuendela kuvumilia
uvunjwaji huu wa sheria unaofanywa na serikali hii ya CCM na ndio maana
sasa wameamua kuuweka ukweli hadharani na kwa sauti kuu.

*Mheshimiwa Spika,* Kwa mujibu wa randama, Tume iliandaa swali la kura ya
maoni kama sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 ilivyowataka kufanya tangu
Octoba, 2014. Na Tume imesema hivyo kwa mujibu wa nyaraka zake kwa Bunge,
naomba kunukuu tena Randama ya Tume ya Uchaguzi uk.12 *'Tume tayari
zimekutana na kuandaa swali la Kura ya Maoni na kulichapisha kwenye gazeti
la serikali la tarehe 17 Octoba,2014'..*

*Mheshimiwa Spika,* Kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 ,
iliyotungwa na Bunge hili iliweka bayana muda maalum wa kuchapisha swali la
kura ya maoni, kutoa elimu kwa umma na siku ya kufanyika kwa kura ya maoni.
Kwa masikitiko ni kuwa muda wa kufanya yote hayo kwa mujibu wa sheria ya
kura ya maoni umeshapita tayari.

*Mheshimiwa Spika,* Sasa ni dhahiri na ni ukweli mtupu kwa mujibu wa sheria
ya kura ya maoni kuwa *, Haiwezekani tena kwa kura ya maoni kufanyika sasa
au baadaye bila kwanza sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 kuletwa hapa
Bungeni kwa ajili ya kurekebishwa ili kuruhusu kura hiyo ya maoni kufanyika
.*

*5.2 Elimu kwa Umma juu ya kura ya Maoni ni utata mtupu:*

*Mheshimiwa Spika, *Jukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu kura ya maoni ni
jukumu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na asasi ambazo zimeidhinishwa
na Tume kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni, na sio jukumu la Serikali .

*Mheshimiwa Spika,* Kwa kipindi kirefu sasa tumeshuhudia kwenye baadhi ya
vyombo vya habari na hasa Magazeti, Redio na Television wakiendelea na
vipindi vya elimu juu ya kura ya maoni na msisistizo mkubwa ni kupiga kura
ya ndiyo ya Katiba Pendekezwa , na hata kwenye maadhimisho ya miaka 51 ya
Muungano kwaya ya vyombo vya dola ambayo ilishirikisha Jeshi, Polisi na
usalama wa Taifa , na wao kwenye wimbo wao ambao waliimba mbele ya Rais
Kikwete waliweka msisitizo wa kupiga kura ya ndiyo kwenye katiba
pendekezwa, ilihali hivi ni vyombo vya dola na ambao havipaswi kufanya kazi
hiyo ya kushawishi umma kufanya uamuzi ambao wanautaka wao na walioandaa
kwaya hiyo.

*Mheshimiwa Spika,* Hatujashangazwa na taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
iliyoko kwenye randama yake kuwa haijawahi kupokea fedha kwa ajili ya
kuendesha zoezi la kura ya maoni ,na hii ni kutokana na ukweli kuwa kura
hiyo ya maoni haiwezekani kufanyika kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni,
na hii inathibitishwa na randama ya Tume ambao uk 12 wanasema kuwa, naomba
kunukuu *'kwa upande wa maandalizi ya kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu, 2015
Tume hatujapokea fedha hadi sasa' .*

*Mheshimiwa Spika,* *Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,*inataka kufahamu ni
nani anayegharimikia gharama za matangazo hayo na fedha hizo zimetoka
kwenye kasma au fungu lipi la bajeti?Je? anayefanya kazi hiyo amesajiliwa
na Tume kwa mujibu wa sheria ? Na kama siyo ni kwanini Tume imeendelea
kukaa kimya huku sheria ya kura ya maoni ikiendelea kuvunjwa ? Ofisi ya
Waziri Mkuu imeshachukua hatua gani mpaka sasa kuzuia uvunjwaji huo wa
sheria ya kura ya maoni?



*5.3 Sherehe za Muungano wa miaka 51 na Kura ya Maoni ya Katiba :**Mheshimiwa
Spika,* *Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, *Tunajiuliza , hivi wale
waliokuwa kwenye ile kwaya iliyokuwa uwanja wa Taifa na kutambulishwa kuwa
ni kutoka vyombo vya dola , bado ni askari wetu na ambao tunategemea kuwa
sehemu ya kusimamia haki kama hiyo kura ya maoni itafanyika ? Serikali
imeweka utaratibu gani wa kuhakikisha kuwa wale wote ambao waliweka msimamo
wao hadharani kuwa kura ya maoni ni lazima kila mwananchi *akapige kura ya
ndiyo; *kama walivyoimba uwanja wa taifa; wanaondolewa kwenye utaratibu
mzima wa kuwa sehemu ya wasimamizi wa kura ya maoni? Haki iko wapi kama
hawa ndio vyombo vyetu vya dola, ambao wanaopaswa kutokufungamana na upande
wowote wa kisiasa kwa mujibu wa sheria ?

*5.4 Tume ya Uchaguzi imeweka msimamo kuwa Hakuna kura ya Maoni bila sheria
kurekebishwa na Bunge :*

*Mheshimiwa Spika,* Pamoja na madhaifu yote ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ,
kuna jambo moja ambalo walau Tume wamekubaliana nasi kama Kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni , wananchi, wanaharakati na viongozi wetu wa dini na hasa
Shura ya Maimamu na wale wa Kikristo, nalo ni kuhusu '*kutokuwezekana
kufanyika kwa kura ya maoni katika wakati huu *kutokana nasababu za
kuvunjwa na ama kuwa na sheria ambayo haieleweki na haitekelezeki.

*Mheshimiwa Spika,* Kwa mujibu wa randama ya Tume uk 14, nanukuu kipengele
cha 2.6 kuhusu Changamoto , wamesema kuwa *'Sheria ya kura ya maoni ina
maeneo ambayo hayawezi kutekelezeka na baadhi yake kuwa na tafsiri zaidi ya
moja .Eneo ambalo linaweza kuleta utata ni Uhesabuji wa Kura ya Maoni na
Utangazaji wa Matokeo'*

*Mheshimiwa Spika,* Tume Imependekeza kuwa ili kura ya maoni iweze
kufanyika ni lazima sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 irekebishwe
kwanza na Bunge , kifungu cha 2.7 cha randama, suluhisho la Changamoto uk
14 kinaeleza kuwa ili kura hiyo iweze kufanyika ni lazima *'Sheria ya Kura
ya Maoni ifanyiwe Marekebisho kwenye maeneo ambayo hayatekelezeki au kuwa
na tafsiri zaidi ya moja'*

*Mheshimiwa Spika*, Huu ni ukweli mchungu ambao Bunge hili linapaswa
kuuchukua kwani Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, tumekuwa tukilalamika juu
ya utaratibu wa Bunge na ambavyo tumekuwa tukitunga sheria zetu mbalimbali
hapa Bungeni japo mapendekezo yetu yamekuwa yakitupwa au kutokusikilizwa
kutokana na mantiki yake na madhara yake ni haya ya kutunga sheria ambazo
hazitekelezeki , mbovu na ni aibu kwenu ambao mara zote mmekuwa mkipiga *kura
za Ndiyo* bila kujali hoja yenyewe , hii ni aibu kubwa kwenu na
mmelisababishia taifa aibu kubwa!

*Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni* , inakubaliana na ukweli huu kuwa kura ya
maoni haiwezi kuwepo mwaka huu wa fedha bila kwanza sheria kurekebishwa
Bungeni na ndio maana hata kwenye maombi ya fedha yaliyoletwa na Tume
katika mwaka huu wa fedha 2015/2016 haikuomba kiasi chochote cha fedha kwa
ajili ya kura ya maoni

*5.5 Msimamo wa Tume, hakuna kura ya maoni ni wa Kikatiba na uheshimiwe !*

*Mheshimiwa Spika, *Kwa mujibu wa Katiba yetu ibara ya 74 (7) imeweka wazi
kuwa Tume ya Uchaguzi ni idara huru inayojitegemea ,itafanya maamuzi yake
rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa vikao vyake . Kwa
mujibu wa Katiba ibara ya 74(11)imeweka wazi kuwa*"katika kutekeleza
majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya katiba hii,Tume ya Uchaguzi
haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya
serikali , au maoni ya chama chochote cha siasa"* *Hivyo basi ni imani ya
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni* kuwa , kwa kuwa Tume ya Uchaguzi imeshakaa
kwenye Vikao vyake kwa mujibu wa Katiba na kuweka wazi vipaumbele vyake kwa
mwaka wa fedha 2015/16 ambavyo vinapatikana kwenye randama yake uk 15 .
Kura ya maoni siyo moja ya vipaumbele vyake kwa mwaka huu wa fedha , Hivyo
basi ni imani yetu kuwa viongozi wa serikali na CCM wataheshimu maamuzi
haya ya Tume na kamwe hawataiingilia Tume katika kutekeleza vipaumbele
vyake kwa mujibu wa Katiba kama ilivyojiwekea katika mwaka huu wa fedha .
Hatutaki kuamini kuwa Waziri Mkuu anaweza kuendelea kuwa sehemu ya kuvunja
Katiba na kulazimisha kura ya maoni ambayo hata hivyo kwa upande wa
Zanzibar hata sheria ya kura ya maoni haijawahi kujadiliwa na kupitishwa na
Baraza la wawakilishi, na hata kama ingepitishwa tunategemea kuwa wananchi
wa Zanzibar wafanye kura ya maoni ili kuruhusu kura hiyo kufanyika kwa
upande wa Zanzibar kwa Mujibu wa katiba yao kama ilivyorekebishwa mwaka
2010.

*6. **MAPITIO YA BAJETI YA SERIKALI MWAKA 2014/15 NA UTEKELEZAJI WAKE.*
*6.1 **FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO.*

*Mheshimiwa Spika,* Kwa mujibu wa randama za wizara na idara mbalimbali za
Serikali ni kuwa Fedha zilizoidhinishwa na Bunge hili kwa ajili ya miradi
mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2014/15 zimetolewa chini ya
kiwango cha asilimia 40 na maeneo mengine kukosa kabisa fedha kwa ajili ya
miradi iliyokuwa imeidhinishiwa bajeti na Bunge hili. Eneo linaloonekana
kupokea fedha yote iliyopitishwa na Bunge kwa ajili ya Maendeleo kwa
asilimia 100 ni fungu 30 Ofisi ya Rais Ikulu eneo la '*Ukarabati Ikulu'* ambapo
zilidhinishwa jumla ya shilingi bilioni 10 na zote zilikuwa zimeshatolewa
na Hazina na kutumika hadi mwezi Machi, 2015

*Mheshimiwa Spika*, Maeneo muhimu kama Vile *fungu 40 Mahakama ya
Tanzania* iliyokuwa
imeidhinishiwa na Bunge hili jumla ya shilingi bilioni 40 walikuwa
hawajapewa hata senti moja na Hazina kwa ajili ya maendeleo hadi mwezi
Aprili ,2015 . Maeneo mengine ambayo yaliidhinishiwa fedha na ambayo
yalikuwa hayajapokea ni pamoja na fungu 16 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali iliyoidhinishiwa bilioni 5, fungu 41 wizara ya sheria na Katiba
,Fungu 37 Ofisi ya Waziri Mkuu ,Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali
iliyoidhinishiwa Bilioni 1.

*Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,* inataka kupata majibu ya Kina ni kwanini
maeneo muhimu kama Mahakama hayakupatiwa fedha zilizokuwa zimeidhinishwa na
Bunge hili? Hivi kipaumbele chetu ni kukarabati Ikulu kwanza au ni
kuziwezesha Mahakama zetu kuwa bora na ili haki iweze kutendeka kwa
wananchi wetu? Ni lini serikali itaweka utamaduni wa kuheshimu muhimili huu
muhimu wa Dola? Kama bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha haikutekelezwa, hivi
kuna maana gani kwa Bunge hili kuendelea kukaa hapa kwa gharama za walipa
kodi kupitisha Bajeti ambayo mwisho wa siku haitatekelezwa na serikali hii
ya CCM? Waziri Mkuu unaisimamia serikali ambayo haiheshimu maamuzi ya Bunge
?

*7. **BAJETI YA SERIKALI 2015/16 NA HALI YA UCHUMI WA TAIFA.*

*Mheshimiwa Spika, *Serikali ya CCM ili kuweza kupata fedha ambazo imeweka
kwenye bajeti yake imeamua kukopa katika mabenki ya Ndani karibia shilingi
Trilioni 6, maana ya hatua hii ya serikali ni kuwa itapunguza mzunguko wa
pesa ambazo mabenki ya kibiashara, yangekopesha sekta binafsi kwa ajili ya
uzalishaji na biashara ambayo ni muhimu kwa ukuwaji wa uchumi na ajira. Badala
yake hizo pesa sasa zinapelekwa serikalini zikatumilke kulipia matumizi ya
kawaida yasiyo ya maendeleo. Kwa maneno mengine Serikali imeamua kuiua
Sekta binafsi kwa kuweka ushindani wa moja kwa moja kwenye kugombania
mikopo kutoka kwenye mabenki ya ndani.

*Mheshimiwa Spika ,* Hali hii inatokana na serikali kutumia zaidi ya uwezo
/kipato chake! NI hali ambayo itaenda kuongeza deni la ndani na hii
inatokana na serikali kushindwa kupata au kukopa fedha toka kwa mabenki na
wafadhili wa nje (Development partners) kutokana na mahusiano mabaya na
hasa yaliyosababishwa na kukithiri kwa vitendo vya kifisadi .

*Mheshimiwa Spika, *Madhara mengine ya hatua hii ya serikali ni Riba
kupanda kwa wakopaji kutoka sekta binafsi maana umepunguza fedha kwenye
mabenki na hivyo kufuatia mahitaji, bei za mikopo (riba) zinaweza kupanda
japo hata sasa ziko juu sana, na kumekuwa na malalamiko mengi toka sekta
binafisi kwamba riba za mikopo kwa ajili ya uzalishaji na uwekezaji ziko
juu. Hii itapelekea mambo kuwa magumu zaidi na zaidi kwa wakopaji wa ndani.

*Mheshimiwa spika ,* Kwa miaka ya siku za karibuni, nchi yetu imekuwa na
utamaduni wa kukopa kutoka mfumo wa kibenki (Benki Kuu na Benki za
Biashara) kama njia ya uhakika ya kufidia nakisi ya bajeti yake . Ukopaji
huu si tu unadidimiza ukuaji wa sekta za uwekezaji na uzalishaji kama
ilivyoelezwa hapo juu, bali pia unaipa Benki Kuu wakati mgumu wa kusimamia
ujazi wa fedha katika uchumi. Pia, kupanda kwa riba kutokana na mabenki
kuwa na fedha kidogo kunaweza kusababisha sekta zisizokuwa na uwezo wa
"ku-break even" kwa muda mfupi hasa sekta ya kilimo na viwanda kudidimia
zaidi.

*Mheshimiwa Spika,* Kutokana na 'risk' na gharama ya mabenki kukopesha
sekta binafsi ni wazi kuwa mabenki mengi yatapendelea kukopesha serikali
kwa kuwa 'risk' ya kupoteza ni ndogo sana. Na kwa kuwa tofauti kati ya riba
zinazotolewa kwenye akiba ni kidogo kuliko zinazotolewa na serikali kwenye
uwekezaji wa hati fungani, mabenki mengi kwa kuwa 'risk averse' zitawekeza
kwenye hati fungani za serikali. Haya ni mabenki, mbali na kuwa na riba za
juu zimekuwa zikisita kukopesha sekta binafsi kwa kuhofia usalama, hivyo
hapa zitapata mteremko wenye gurantee ya usalama.

*Mheshimiwa Spika ,* Kutokana na Serikali kukopa kwenye mabenki binafsi
katika riba ya soko (isiyo na unafuu) ili kujalipa baadae, hiyo itapelekea
deni la serikali kueindelea kuwa kubwa, jambo ambalo halitakuwa tu msalaba
kwa Taifa na Watanzania, bali deni hilo litawaogopesha wawekezaji na
wakopeshaji wa nje kama serikali ita-default katika urejeshaji wa mikopo
hiyo.

*Mheshimiwa Spika,* Ni kweli kuwa kwa mujibu wa takwimu, Uchumi unakua na
kwa sasa ni takribani asilimia 7, lakini umasikini umebakia pale;
inequality imeongezeka na ajira hasa kwa vijana zimepungua sana. Takwimu za
hivi karibuni zilizotolewa na Wizara ya Fedha na Benki ya Dunia inaonyesha
umasikini bado uko juu kwani umepungua kidogo sana toka asilimia 34 mwaka
2007 mpaka asilimia 28 mwaka 2012, na umebadilika kwani masikini wengi wa
vijijini wanahamia mijini. Hizi takwimu za serikali zikifanyiwa uchambuzi
huru hali ya umasikni na inequlity unaweza kuwa mbaya zaidi. Kwa ufupi,
matunda yanaliwa na wachache walioko kwenye sekta zinazokua zaidi (utalii,
biashara, madini, viwanda, etc.) wale walioko kwenye sekta ya kilimo cha
jembe la mkono (75%) inayokua taratibu ukilinganisha na ukuaji wa jumla,
wana njia ndefu ya kwenda, umaskini unakithiri!

*Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,* inataka kupata majibu ya kina serikali
imejipanga vipi kuondokana na utaratibu huu wa kuwa na bajeti kubwa kwenye
makaratasi wakati kiuhalisia haina uwezo wa kuitekeleza bajeti hiyo? Aidha,
kuna mkakati gani wa kuhakikisha kuwa inawanusuru wawekezaji wa ndani na
riba kubwa kutokana na serikali kuamua kukopa kwenye sekta za ndani za
fedha ? Ofisi ya Waziri Mkuu ina mikakati gani ya kukuza ajira na kuwezesha
sekta binafsi kuweza kuzalisha?

*8. **MAMLAKA YA USTAWISHAJI MAKAO MAKUU-CDA* *Mheshimiwa Spika,* CDA ni
mamlaka ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1972 na hivi sasa ina umri wa miaka
43 katika utendaji kazi wake wa jukumu la kwanza lilikuwa ni kuhakikisha
kuwa Mji wa DODOMA ardhi yake yote imepimwa.

*Mheshimiwa Spika, *Kwa mujibu wa Randama Fungu 37 Uk. 126 inaonesha kuwa
kwa mwaka wa fedha 2014/15 mamlaka kupitia Mradi wa Uboreshaji Miji(TSCP)
ilitengewa jumla ya Tshs.206,744,000/- kwa ajili ya kujenga uwezo wa
Taasisi. Kambi Rasmi ya Upinzani inajiuliza Taasisi yenye miaka 43 na
ambayo inakusanya kodi za nyumba na viwanja kwa muda wote huo inapokeaje
fedha za kujengewa uwezo?

*Mheshimiwa Spika*, CDA kama mamlaka ya kuendeleza makao makuu imekuwa ni
tatizo kubwa sana kwa wakazi wa Mji wa DODOMA, kwa zaidi ya miaka 42 ya
uwepo wake, Mamlaka haijakamilisha jukumu lake la kwanza la kupima viwanja
maeneo yote ya mji ili kufanya ujenzi ufuate utaratibu utakao wekwa.

*Mheshimiwa Spika, *Kabla ya CDA kuanzishwa na baada ya kuanzishwa,
wananchi wa Dodoma walikuwa wanaishi katika maeneo yao na wanaendelea
kujenga na kuishi kwa sababu hakuna mipaka ya ardhi iliyowekwa na CDA.
Lakini CDA wanapotaka kupima eneo Fulani ambalo tayari lina makazi ya
wananchi hutoa notice na kuwataka wakaazi wa eneo husika kubomoa nyumba zao
wenyewe bila ya fidia.

*Mheshimiwa Spika, *Inapotokea wananchi wanaposhindwa kubomoa nyumba hizo
kutokana na kukosa mahali pa kwenda ,CDA hubomoa na kuwadai wananchi hao
gharama za kubomoa nyumba zao. Maeneo ambayo yamebomolewa nyumba zao na CDA
ni pamoja na : Ndejengwa mwaka 2012 ambapo zilibomolewa nyumba 127, Eneo la
Itega mwaka 2013, Msangalalee kata ya Makaru mwaka 2014 nyumba 35 n.k.

*Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,* inataka kujua ni lini uonevu huu kwa
wananchi wa Dodoma utasitishwa na serikali hii ya CCM? Maana wimbo wa Makao
makuu kuwa Dodoma unaonekana umekosa mchezaji na mamlaka hii haionekani
ikiwa tayari kufanya jukumu lake la msingi la kuanzishwa kwake .

*9. **IDARA YA MPIGA CHAPA MKUU WA SERIKALI*

*Mheshimiwa Spika*, Idara hii ni idara muhimu sana kama ingetumika vyema na
kama Serikali ingekuwa na nidhamu ya kutokuingilia utendaji wa Idara ambazo
ziko chini yake. Kwani gharama kubwa zinazoingiwa na taasisi na Idara za
Serikali katika kuchapa nyaraka mbalimbli ni kubwa mno. Mheshimiwa Spika,
Ukiangalia Randama fungu 37 uk.3 kuhusu kupungua kwa maduhuli kuwa ni
kutokana uchakavu wa mitambo ya uchapaji ya Idara ya Mpigachapa Mkuu wa
Serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema hii ni aibu kubwa kwa Serikali
kwani ofisi ambayo ni tegemeo katika kuliingizia Taifa fedha inawezekanaje
kushindwa kununua vitendea kazi wakati inazalisha fedha za kutosha?

*Mheshimiwa Spika, *Kwa mwaka wa fedha 2014/15 Idara ilitengewa fedha za
ndani Tshs.1,000,000,000/- kwa ajili ya Programu ya kuimarisha Idara hii,
lakini kwa kuwa Serikali ya CCM haioni umuhimu wa Idara hii hadi mwezi
Machi, 2015 hakuna hata senti moja ambayo Idara imepokea kwa ajili ya
program tajwa. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha Idara hii
imepangiwa Jumla ya Tshs.500,000,000/- tu. Hoja ni kama mwaka jana
ilipangiwa kupatiwa shilingi bilioni moja na sasa thamani ya shilingi
imezidi kuporomoka imepangiwa kiasi pungufu ya nusu ya mwaka jana. Mitambo
inanunuliwa nje ya nchi, Je fedha hizo si zitakuwa ni kwa ajili ya
kufaulishwa kwenda kwenye mipango mingine ambayo si ya kuimarisha Idara
hiyo?

*Mheshimiwa Spika,* Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kama kweli ofisi
hii ikiimarishwa ni dhahiri kusingekuwa na ulazima wowote kwa Serikali
kuingia kwenye Kandarasi za uchapaji wa nyaraka mbalimbali za uchaguzi na
nyingine nyingi. Kwani tunaamini katika ushindani wa Zabuni hizo Idara
ingeshinda kwa kuwa kuna ruzuku ya Serikali katika uendeshwaji wake. Hili
lingewezekana pale tu dhana nzima ya Utawala Bora itakapotekelezwa kwa
vitendo na wananchi kuona kwamba utawala bora upo katika utendaji wa
Serikali. Mabilioni ya fedha za Walipa kodi yangeokolewa na pia
kusingekuwepo na ucheleweshaji wa kazi kwaajili ya watendaji waandamizi wa
Serikali kudai kwanza 10% kabla ya kazi kutolewa, jambo linaloturudisha
nyuma.

*10. **MAPENDEKEZO YETU YA NYUMA NA AHADI ZA SERIKALI* *10.1 **RERA (Real
Estate Regulatory Authority)*

*Mheshimiwa Spika,* Katika hotuba yangu ya mwaka wa fedha 2011/2012
niliitaka serikali kuanzisha chombo kitakachoweka uratibu na usimamizi wa
sekta ya majengo makubwa ya biashara inayokuwa kwa kasi kubwa. Mamlaka hii
siyo tu itasimamia haki za wapangaji, bali hata mapato ya Serikali na ubora
wa majengo haya na huduma zake. Nilipendekeza mamlaka hii ya udhibiti iitwe
"Real Estate Regulatory Authority." Tunarudia tena kusisitiza ushauri wetu
huu kwani Serikali inapoteza mapato bila sababu ya msingi kwa jeuri na
kiburi cha kutokubali ushauri uliotoka upinzani.

*10.2 **Uundwaji wa Tume Huru za Kimahakama*

*Mheshimiwa Spika,* Kumbukumbu za taarifa rasmi za Bunge zinaonyesha kwamba
katika hotuba yangu ya mwaka 2011/2012 tuliishauri Serikali kuhusu kuunda
tume ya kijaji ya uchunguzi wa vifo vya raia. Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walikubali na wakaahidi kutekeleza hilo,
lakini toka mwaka huo hadi sasa hakuna chochote kilichotekelezwa na
Serikali hii ya CCM.

*Mheshimiwa Spika,* Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba Serikali haina
dhamira yeyote ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hili ambalo wananchi
wamekuwa wakililalamikia kuhusu jamaa zao kuuawa na vyombo vya dola. Ni
ukweli uliowazi kwamba tangu kipindi hicho vimeripotiwa vifo kadhaa, majina
ya watu waliouawa yanapatikana katika taarifa ya haki za binadamu ya mwaka
2013, uk. 22.

*10.3 **UNUNUZI WA SAMANI ZILIZOTENGENEZWA NCHINI*

*Mheshimiwa Spika,* Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na msisitizo kuhusu ofisi
na taasisi za serikali kununua samani zinazotengenezwa nchini. Ni dhahiri
kuwa nchi zilizoendelea hazikufanikiwa kupiga hatua bila kushirikiana na
wafanyabiashara wa ndani hivyo samani za ndani zikinunuliwa kwa wingi pato
la taifa litaongezeka kwani lita – stimulate sekta nyingine za uchumi
ikiwemo ajira. Serikali lazima sasa ieleze ni wizara, taasisi na ofisi zake
ngapi zimeanza kutekeleza tamko la Serikali la kuanza kutumia samani
zilizozalishwa na viwanda vya ndani ya nchi , pamoja na ahadi za Waziri
Mkuu hapa Bungeni?

*10.4 **Gharama kubwa za uendeshaji wa Serikali*

*Mheshimiwa Spika,* Kama Serikali ingekuwa inajali gharama basi ingekuwa
inafanyia kazi mapendekezo ya Kambi ya Upinzani tangu mwaka 2011 ambapo
tuliishauri kupunguza matumizi ya kawaida na kuongeza fedha katika miradi
ya Maendeleo. Aidha, Serikali ingeacha kuendelea kugawa mikoa na Wilaya
kwani kwa kufanya hivyo ni kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali. Ni
jambo la ajabu kabisa kwamba kwa jinsi Serikali hii isivyojali gharama za
uendeshaji wa Serikali, hata Kata ya Mbagala sasa inapendekezwa kuwa Wilaya
Mpya!!! Ofisi ya Waziri Mkuu imeshindwa kumshauri Rais juu ya ugawaji wa
Mikoa na Wilaya, matokeo yake kila kukicha tunajenga Makao Makuu ya Wilaya
na Mikoa wakati fedha hizo tungeweza kuzielekeza kwenye miradi ya Maendeleo
na huduma za jamii kama vile shule, hospital , hata Tume ya Uchaguzi
imelalamikia jambo hili kuwa linawavuruga sana katika kuweza kupanga
mipango yake kama kuweka mipaka ya majimbo na Kata kwa mujibu wa sheria .

*10.5 **Sherehe za Kitaifa*

*Mheshimiwa Spika, *maadhimisho hayo yote hufanyika kuanzia ngazi ya Taifa
hadi ngazi ya Wilaya kwa kufanya sherehe mbalimbali zinazohusisha viongozi
wa kiserikali, na hivyo ni dhahiri matumizi ya kodi za wananchi hutumika.
Kambi ya Upinzani inasema kuwa matukio hayo ya kihistoria ni muhimu
yaeleweke kwa vizazi vyetu vya sasa na vijavyo.

*Mheshimiwa Spika*, katika kufikia azma hiyo *si lazima* tutumie fedha
nyingi za walipa kodi wakati Serikali inashindwa kutimiza wajibu wake
muhimu zaidi wa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake, kama vile huduma
ya maji safi na salama, elimu bora kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya
juu, kupeleka nishati kwenye maeneo ya uzalishaji na kwa Watanzania waishio
vijijini n.k.

*Mheshimiwa Spika, *Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali badala ya kufanya
maadhimisho ya Sherehe hizo zote tuchague ni sherehe zipi zinatoa tija kwa
Watanzania na zipi hazileti tija na maadhimisho yake yaweke kwenye
kumbukumbu za kihistoria. Hoja yetu hiyo imeungwa mkono katika taarifa ya
Utekelezaji wa Majukumu pamoja na Bajeti ya Matumizi ya kawaida na Mpango
wa maendeleo ya Mwaka 2013/14, 2014/15 na Makadirio ya mwaka 2015/16 ya
Mkoa wa RUKWA fungu 89 uk. 15 Nanukuu *"Kuongezeka kwa vikao, mikutano na
makongamano yanayoitishwa na ngazi za Kitaifa kwa maagizo ya kugharamiwa na
Mikoa na Halmashauri, ambayo hayapo katika bajeti za mikoa na Halmashauri,
katika mazingira ambapo Mikoa na Halmashauri haina fedha za kutolea hata
huduma za msingi kwa wananchi" *Hiki ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya
Taifa* .*

*10.6 **Pension kwa Wazee*

*Mheshimiwa Spika*, Kambi ya Upinzani wakati tunawasilisha hotuba yetu
mwaka 2011/2012 tulisema yafuatayo, nanukuu:

*"**Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa dhana ya hifadhi ya jamii ni pana sana,
Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kuzingatia pendekezo letu kuweka mfumo
utakaowafanya wazee wote kupata pensheni (Universal pension) kila mwezi ili
kuwapunguzia wazee wetu hasa waishio vijijini gharama kubwa za
maisha".** Mwisho
wa kunukuu.*

*Mheshimiwa Spika, **Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa pensheni hii ni
muhimu kwa kuwa itasaidia kuongeza kipato kwa wanaoishi vijijini ambako
umasikini wa kipato umejikita na kupunguza umasikini kwa kiwango cha
takriban asilimia 57.9 kwa wazee walio na umri zaidi ya miaka 65.*

*11.0 SERIKALI KUPUUZA NA KULIDANGANYA BUNGE*

*Mheshimiwa Spika,* Taifa hili limekuwa mhanga wa mara kwa mara wa uzembe
au kudanganywa na hata kupuuzwa kwa maazimio ya Bunge, ambalo kikatiba,
ndilo lenye wajibu wa kuisimamia Serikali. Kupuuzwa huku kwa Bunge,
kunadhalilisha uwepo wa taasisi hii nyeti ya Taifa, kunaondoa uwajibikaji
wa Viongozi na watumishi wa Serikali na hatimaye kunalisababishia Taifa
hasara kubwa siyo tu kiuchumi katika maeneo yanayohusu musuala ya kiuchumi,
bali pia katika upatikanaji haki katika Taifa.

*Mheshimiwa Spika,* Wakati Dunia inajua vilivyo kwamba Bunge lilifanya kazi
yake katika kuisimamia serikali, juu ya kashfa ya Operesheni Tokomeza na
mwishowe kuishia kwa mawaziri wanne kuachia madaraka kwa kuwajibika
kisiasa, leo serikali inarudi kwa mlango wa nyuma na kudai eti hakukuwa na
tatizo. Aidha, Serikali imeendelea kufanya mkakati wa makusudi wa kuficha
uovu na uzembe kwa kusafisha viongozi katika masuala yote yanayohusu umma
hususan pale viongozi wa serikali na familia zao wanapokuwa ni wahusika
wakuu katika kashfa husika. Kwa mfano, Serikali imeshindwa hadi leo kuweka
hadharani ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais ya majaji watatu; Jaji Hamisi
Msumi (Balozi) akiwa mwenyekiti; Jaji Stephen Ernest na Jaji Vincent
Kitubio ikiwa imekabidhi ripoti yake serikalini na badala yake kutangazwa
na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Kwa mfano, Balozi Sefue
anasema mawaziri wote wanne waliojiuzulu mwaka 2013 kwa sakata la
Operesheni Tokomeza hawana hatia. Yaani serikali inataka hata kusema kwamba
hata kule viongozi hao kuchukua wajibu wa kisiasa kuwajibika ni kinyume cha
utawala bora. Wakati ikisema hivyo, serikali hii ya CCM inakubali kwamba
kuna watu waliuawa kwa makosa, idadi ya ilikuwa inaonyesha ni watu 15
ingawa Tume inathibitisha vifo tisa; Tume inakiri kwamba kuna watu
walidhalilishwa; kuna watu waliharibiwa nyuma na mali zao kama mifugo
kupigwa risasi na kila aina ya uonevu. Serikali imekubali kulipa fidia kwa
wote waliokumbwa na madhila haya. Katika mazingira haya uwajibikaji wa
kisiasa unakuwaje kosa? Serikali inasafisha vipi waliowajibika kisiasa?

*Mheshimiwa Spika,* Kwa nini hatujifunzi kwa Mzee wetu, Rais Mstaafu Ali
Hassan Mwinyi, alipowajibika miaka ya sabini kwa sababu ya madhila
waliotendewa wananchi na askari ingawa yeye mwenyewe hakushiriki. Serikali
hii kwa nini inaogopa na kukwepa uwajibikaji? Kama serikali hii inaamini
katika uwajibikaji na uwazi iweke hadharani ripoiti ya Majaji watatu kuhusu
kashfa ya Operesheni Tokomeza ili wananchi waisome na kujiridhisha
vinginevyo serikali hii inaendeleza tabia ile ile ya kukwepa kuwajibishwa
na Bunge kama ilivyokuwa kwenye maazimio ya Operesheni Tokomeza.

*Mheshimiwa Spika,* Juhudi za serikali za kutaka kusafisha na kufunika
kashfa zake pia kumethibitika wiki iliyopita tu baada ya Katibu Mkuu
Kiongozi tena kujaribu kuwasafisha wahusika wa sakata la Tegeta Escrow.
Watanzania wanajua na dunia inajua kwamba kama kuna wizi wa mchana kweupe
umefanyiwa nchi hii ni kashfa ya Tegeta Escrow, watumishi wa umma
wamehongwa mamilioni ya fedha, majina yametajwa; aliyekuwa Katibu Mkuu
Nishati na Madini, Eliackim Maswi na Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo,
walionyesha ni kwa jinsi gani walishindwa kuisaidia serikali na nchi
isiibiwe kwenye kashfa hii, lakini pamoja na maazimio ya Bunge kuwataja kwa
ushahidi jinsi walivyoshindwa kutekeleza majukumu yao, serikali imekuwa
hailali eti ikitafuta njia ya kuwasafisha. Hii ni serikali pekee duniani
inayokasirika Bunge likifanya kazi yake sawa sawa ya kuisimamia ndiyo maana
mara nyingi imegeuka na kutafuta njia ya kufunika madudu ambayo siyo tu
yameiaibisha sana, bali yamegharimu kodi nyingi za wananchi. Serikali
inajua kwamba utekelezaji wa bajeti ya serikali inayomalizika ya mwaka
2014/15 umekwamishwa sana na kashfa ya Tegeta Escrow baada ya nchi
wafadhili kuzuia kutoa fedha za kuchangia fungu la maendeleo kutokana na
tabia ya serikali kufunika kombe mwanaharamu apite kwenye kashfa hii.
Tunataka serikali iseme kwamba inapolinda na kubeba wahusika wa kashfa hizi
wanataka kuwasaidia wananchi au viongozi wameamua kujiunga dhidi ya
wananchi wao? Serikali inajua kuwa kashfa ya Escrow ina mizizi katika
kashfa ya IPTL iliyoanza mwaka 1994 ndani ya Wizara ya Nishati na Madini
Rais Jakaya Kikwete akiwa waziri, ikaidhinishwa mwaka 1995 Rais Jakaya
Kikwete akiwa Waziri wa Fedha na sasa inafumuka katika sakata hili la
Escrow na kuiparaganyisha serikali Rais Kikwete akiwa madarakani. Ni kwa
nini mambo haya yanatokea na serikali inaendelea kuyabeba na kusafisha uoza
huu? Ni kwa faida ya nani?

*Mheshimiwa Spika,* Kamato Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mhe. Christopher
Ole Sendeka ilitoa mapendekezo muhimu na mazuri wa namna ya kukabiliana na
kutatua migogoro yo muda mrefu ya Wakulima na Wafugaji. Hadi sasa Serikali
haijaeleza kinagaubaga imejipanga vipi kutekeleza maazimio haya ya Bunge,
lakini tunashuhudia wakulima na wafugaji wakiendelea kupambana na
kuharibiana mali na hata kuuana,

*Mheshimiwa Spika,* Katika mlolongo huu wa kushindwa kusimamia nchi,
kuendekeza makundi na vita vya kisiasa ndani ya CCM na serikali yake kwa
gharama ya Taifa, taifa hili sasa linadaiwa Sh. bilioni 120 baada ya
kushindwa kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika Mahakama ya Kimataifa ya
Usuluhishi (ICC) huko Paris. Serikali haijataka kuliweka jambo hili wazi na
ni dhahiri kuna siri kubwa inayosababisha jambo hili kuwa la usiri mkubwa.
Huko mbele ya safari jambo hili litaligharimu Taifa mabilioni haya ya fedha
ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala mchakato
mzima wa kashfa ya Richmond. Serikali isimame sasa na ilieleze Taifa ni
nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani analindwa na
serikali katika kashfa hii?

*Mheshimiwa Spika,* Mapambano ya mitandao ndani ya serikali ya CCM na
minyukano ya kupigania maslahi na ulaji ndani ya mikataba mbalimbali ya
miradi ya umma ikiongozwa na walio karibu na Watawala na familia zao imeota
mizizi katika serikali hii.

*Mheshimiwa Spika,* Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kujua kwamba
serikali hii ya CCM ambayo imefikia mwisho wake ni kwa nini inawaachia
Watanzania madeni makubwa hivi? Je, kashfa hizo zote za serikali kushindwa
kuwajibika, kutafuta visingizio vya kufunika madhambi yake, ndiyo maisha
bora kwa kila Mtanzania ambayo wananchi waliahidiwa miaka 10 iliyopita?
Nini kauli ya serikali juu ya tabia hii ya kuwabebesha wananchi mizigo ya
madeni huku serikali hiyo hiyo ikijitahidi kwa nguvu zake zote kuwasafisha
viongozi walioitumbukiza nchi kwenye madhila haya? Ni jambo la kumshukuru
Mungu kuwa sasa hatimaye utawala wa CCM unakaribia ukingoni na ni rai yangu
kwa Watanzania wote waonyeshe hasira yao ya kuibiwa, kudhalilishwa na hata
kufanywa mafukara kwa kikinyima chama hiki cha zamani kilichogawana
rasilimali za Taifa hili kwa misingi ya kifisadi kwa muda mrefu.

*TUKUBALIANE KWA PAMOJA KUWA NI KWA MASLAHI YA TAIFA LETU NA VIZAZI VIJAVYO
KUIONDOA CCM MADARAKANI SASA KWANI KASI YA UKWAPUAJI INAZIDI KUSHIKA
KASI*. *Mheshimiwa
Spika, *Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
naomba kuwasilisha.
*……………………………………*
Freeman Aikaeli Mbowe (MB)
*KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI (KUB)*
*12 Mei, 2015*

Comments