Wabunge wawili walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, wameanza rasmi kufanya kazi za kibunge jana, baada ya kupishwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda, kabla ya kuanza kikao.
Hatua hiyo inawapa nafasi wabunge hao kushiriki vikao vilivyosalia, katika mkutano wa 19 wa Bunge la 10 ambalo limebakiza takriban siku tatu za kazi na vikao hivyo vikimalizika kinachongojewa ni Bunge la Bajeti litakalohitimisha uhai wa bunge hilo katika kipindi cha miaka mitano ya kuanzia 2010 hadi 2015.
Uteuzi wa wabunge hao wateule wa Rais Kikwete, Dk. Grace Puja na Innocent Sebba,umepokewa kwa mitazamo tofauti ndani ya jamii, huku bungeni jana kukiibuka maswali, yakiwemo yaliyohoji ikiwa watalipwa kiinua mgongo sawa na ambao wamekuwa wabunge kwa miaka mitano.
Hoja hiyo, ingawa ilienea chini chini miongoni mwa baadhi ya wabunge, iliwekwa hadharani na Felix Mkosamali( Muhambwe, NCCR-Mageuzi), baada ya kuomba mwongozo wa Spika akitaka kufahamishwa uhalali wa uteuzi huo na ikiwa kiinua mgongo cha wateule hao kitakuwa kwa miaka mitano.
"Naomba mwongozo kwa jambo lililotokea asubuhi la kuapisha wabunge wapya zikiwa zimebaki takribani siku 60 hivi, hasa kuhusu madaraka ya Rais yaliyopitiliza ya kuteua watu walipwe mafao na vitu vingine sawa na wabunge wengine waliotumikia taifa kwa kipindi hicho?" alihoji Mkosamali.
Pia alisema kwa msingi wa uteuzi huo, sheria inayoweka muda wa ukomo wa uchaguzi wa wabunge, kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, irejeshwe bungeni na kufanyiwa marekebisho ili, jimbo linapokosa uwakilishi kwa sababu yoyote ile, uchaguzi ufanyike.
Jimbo ya Kigoma Kaskani ambalo mbunge wake, Zitto Kabwe, alijiuzulu na Mbinga Magharibi, ambalo mbunge wake, Kapteni John Komba, alifariki yalitumiwa na Mkosamali kama mifano wa mapengo yaliyopo bungeni, ambayo kwa uteuzi wa wabunge hao nayo yanatakiwa kuzibwa kwa wananchi kufanya uchaguzi.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) George Masaju, alisema uteuzi huo hauna tatizo kwakuwa katiba ya nchi inampa mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi 10, katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake na kwamba haijamuwekea ukomo wa muda wa kutumia mamlaka hayo.
"Katika kutekeleza hilo, Rais hakuwekewa ukomo, ukomo uliowekwa ni kwa uchaguzi wa wabunge wa majimbo...,kwa hiyo uteuzi huu hauna madhara kwa kuwa hata tarehe ya kuvunjwa Bunge haijatangazwa," alisema Masaju.
Kufuatia sintofahamu hiyo, ambayo iliambatana na minong'ong'ono ya hapa na pale, AG aliwaasa wabunge kutumia vizuri fursa ya kutengeneza Katiba ya Nchi, pindi inapopatikana kwa kurekebisha masharti ambayo hawayakubali.
Comments
Post a Comment