SING’OKI MPAKA UCHAGUZI UFANYIKE, ANG’AKA MREMA



SING'OKI MPAKA UCHAGUZI UFANYIKE, ANG'AKA MREMA

Augustine Mrema 

 MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema amesema hawezi kung'oka katika nafasi yake ya uongozi hadi hapo uchaguzi wa chama hicho utakapofanyika.

Uchaguzi wa chama hicho unatarajiwa kufanyika Aprili 26 mwaka huu, huku matarajio ya wanachama hao ni kumng'oa Mrema kabla ya uchaguzi huo kufanyika.

Akizungumza katika mkutano wa Kamati Kuu uliofanyika kwenye Makao Makuu ya chama hicho, Dar es Salaam jana, alisema hawezi kujiuzulu hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika.

Mrema anatuhumiwa na wanachama wa chama hicho kwamba anaongoza kidikteta, kinyume na katiba ya chama pamoja na kuongoza kikabila.

Alisema kwamba makundi ya watu wanaojiita wanachama wa chama hicho waliokwenda kutoa malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, hayatambui na kwamba ni wahuni.

Mbunge huyo wa Vunjo, alisema kwamba makundi hayo ya vijana huwa wanajitokeza wakati wa uchaguzi ili kuchochea fujo katika chama hicho.
"Lazima tuwapige vita vijana hawa wanaojitokeza wakati wa harakati za uchaguzi. Mimi naweza kulifananisha kundi hilo na lile la al Shabaab kwani hatuwatambui kikatiba,''alisema Mrema.

Pia aliongeza kuwa katika chama hicho anaongoza kupitia katiba ya chama na ya nchi hivyo tuhuma hizo dhidi yake hazina nafasi kwa wakati huu.


Comments