ADHABU YA KIFO SI SURUHU KWA WASAFIRISHAJI WA MADAWA



ADHABU YA KIFO SI SURUHU KWA WASAFIRISHAJI WA MADAWA

ABIRIA mmoja ndani ya basi la daladala lililokuwa likipita katika kituo cha basi cha Magomeni Hospitali, Dar es Salam, aliona vijana wawili 'mateja' wakiwa wamelala katika benchi la abiria huku mate yakiwatoka.
Kwa sauti kubwa alisema kuwa wakati umefika wa serikali kuwa na sheria kali hata kama adhabu ya kifo kwa wanaotiwa hatiani kwa makosa ya biashara ya dawa za kulevya. Katika maelezo yake ambayo yaliungwa mkono na karibu nusu ya abiria waliokuwamo ndani ya basi hilo kuwa wafanyabiashara hiyo haramu ni haki 'wanyongwe'.



Abiria mmoja mkereketwa kama si mwanaharakati alisema anaamini adhabu ya kunyongwa kutaifanya Tanzania kuwa salama dhidi ya uingiaji na usambazaji wa dawa za kulevya. Abiria mwingine ambaye alidakia hoja hiyo, alisema anajisikia uchungu kila anapowaona vijana katika vijiwe vyao na mitaani kwani anakumbuka vifo vya watoto wawili katika familia yake waliokufa kufuatia matumizi ya dawa za kulevya.
Akasema mmoja alikuwa ni mtoto wa ndugu yake aliyekufa eneo la Kinondoni, kifo cha ghafla baada ya kutumia dawa nyingi na wa pili alikufa Tandika kwa sababu kama hiyo.
"Watu hawa wanaoingiza dawa za kulevya nchini wanastahili kuwekewa sheria kali hata kama ni kuuawa kwa kunyongwa ili serikali iwamalize na watakaobaki wapate fundisho," alisema abiria huyo ambaye aliitaja nchi ya China kuwa ni moja ya nchi inayofanya vizuri katika kumaliza watu wa aina hiyo, jambo ambalo linatoa fundisho kwa wanaotaka kufanya biashara hiyo.
Katika kuthibitisha kauli yake juu ya hatua zinazochukuliwa na China, anakariri habari katika vyombo vya habari za mwezi Februari mwaka huu ambapo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anne Maembe alisema kuwa China imewahukumu adhabu ya kifo kwa kuwanyonga Watanzania 100 baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kuingiza dawa za kulevya nchini humo.
Abiria huyo aliyejitaja jina baada ya kumuuliza kuwa anaitwa Mntambo anayetokea Tanga, mwalimu na mkulima, alisema Tanzania inayosifika kwa amani umefika wakati wa kuchukua hatua kama ya China mara moja ili kuondokana na fedheha ambayo nchi inapata kwa jinsi dawa za kulevya zinazoingia na kutoka nchini.
"Vijana kama hao ni kama wamekufa tu. Mtu analala mchana kweupe kituoni udenda unamtoka kweli kuna mtu hapo," akawa anasema Mwalimu Mntambo.
Hata hivyo, watu wengine waliohojiwa kwa nyakati tofauti wanapinga hatua hiyo ya adhabu ya kifo kwa wafanya biashara wa dawa za kulevya kwa maelezo kuwa uamuzi wa aina hiyo si suluhu katika kumaliza tatizo hilo Mbunge wa Maswa, John Shibuda anasema kuwa pamoja na ukweli kuwa biashara ya dawa za kulevya nchini zimeleta madhara makubwa nchini, adhabu ya kifo si suluhu.
Yeye anaamini kuwa kwa Bunge kuidhinisha kuwa adhabu ya kifo kwa wafanyabiashara hao kutaongeza madhara zaidi ya kutokea kwa vifo vya ajabu kwa watu mbalimbali ambao watakuwa wakiuawa na wana mtandao wa wafanyabiashara hiyo kwa lengo la kulipa kisasi.
"Tunapoamua kutoa adhabu ya aina hii lazima pia tuchukue tahadhari. Ifahamike kuwa wasafirishaji wa dawa za kulevya ambao wanakabiliwa na kesi zenye muelekeo wa adhabu ya kifo watafanya kila linalowezekana kwa kuwaua wanaowafuatilia ili wasikamatwe, jambo ambalo pia ni la hatari kwa maisha ya watendaji wa vyombo vya usalama," anasema.
Katika maelezo yake kwa njia ya simu ambayo pia aliyatoa katika mchakato wa Bunge la Katiba, Shibuda anasema kwa jinsi maadili ya utendaji kazi nchini yalivyokwenda kombo kutokana na rushwa, ipo hatari utekelezaji wa hukumu ya kifo itakapoanza kutumika ukaambatana na hali ya kulindana na upendeleo, hatua itakayoweza kusababisha watakaohukumiwa kuwa watu ambao si wahusika wa makosa ya biashara ya kulevya.
Maoni ya Shibuda na wengine katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Dodoma na Mbeya yanaungwa mkono na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Duniani (Amnesty International) ambalo lenyewe moja kwa moja hupinga adhabu ya kifo inayotolewa na serikali mbali mbali kwa maelezo kuwa ni kinyume na utoaji wa haki za binadamu.
"Amnesty International inapinga vikali adhabu ya hukumu ya kifo kwa kesi ya aina yoyote kwa misingi kuwa adhabu ya kifo kwa binadamu ni kitendo cha ukatili, kinyama na kisicho cha kibinadamu na kinachovunja haki ya mtu kuishi," linaeleza shirika hilo katika taarifa inayoshauri serikali mbalimbali duniani kufuta adhabu za kifo kwa watuhumiwa.
Shirika hilo linasema katika taarifa yake katika mtandao kuwa lina matumaini kuwa maelezo yake hayo kuwa adhabu ya kifo kwani kitendo cha ukatili, kinyama na kisicho cha kibinadamu na kinachovunja haki ya mtu kuishi kitazifanya serikali zenye kutekeleza adhabu hiyo kubadilika na badala yake kuwa na sheria ambazo si adhabu ya kifo.
Amnesty International inatetea hoja yake hiyo ya kupinga adhabu ya kifo kwa kueleza kuwa hata katika nchi ambazo zinatekeleza adhabu hiyo biashara hiyo inafanyika kwa kiwango kikubwa kuonesha kuwa utekelezaji wa adhabu hiyo si suluhu. Imetoa mfano wa Iran ambako watu zaidi ya 2000 wamenyongwa kwa makosa ya biashara hiyo ya dawa za kulevya nchini humo tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya mwaka 1979.
Lakini pamoja na kutekelezwa kwa adhabu hiyo bado nchi hiyo ndio njia kuu ya kusafirisha heroin kutoka Afghanistan na Pakistan kwenda kwenye masoko ya Ulaya.
China nayo imekuwa ikiendeleza adhabu hiyo ya kifo kwa mamia ya watu wanaogundulika kuwa na dawa za kulevya hususan katika majimbo ya karibu na eneo linalojulikana kama "Golden Triangle", lakini utekelezaji wa sheria hiyo bado haujasaidia sana kwani inaelezwa kuwa wasafirishaji wa dawa hizo wamebuni njia nyingine ya kuingiza heroin nchini humo kwa njia ya anga na reli.
Ni kutokana na hali kama hii, Amnesty International inaamini kuwa kutokuwapo kwa adhabu ya kunyongwa kudhibiti biashara ya dawa za kulevya hakutaathiri juhudi za nchi yoyote katika mapambano ya kukabili tatizo hili, inasema taarifa hiyo.
Abdulrahaman Salim Mkazi wa Mwanagati katika wilaya ya Ilala amesema kuwa serikali lazima ione umuhimu wa kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kwa kuwa matumizi ya dawa hizo yanapotumiwa na akina mama athari zake pia huwapata watoto wanaonyonya jambo ambalo ni hatari kwa taifa hili katika miaka ijayo.
Wiki iliyopita gazeti moja nchini liliandika habari kuwa mtoto wa miezi mitatu aliathirika na dawa za kulevya kwa kunyonya maziwa ya mama yake aliyetajwa kwa jina la Zena. Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Ester Bulaya anasema kutokana na kuongezeka kwa tatizo la dawa za kulevya nchini katika miaka ya hivi karibuni ni muhimu kwa serikali kufanya marekebisho ya sheria ya sasa na kuwa na sheria kali ya kukabiliana na tatizo hili.
Bulaya ambaye alitoa maelezo haya bungeni hivi karibuni aliitaka serikali ifanye mabadiliko/ marekebisho ya sheria ya dawa za kulevya na kuanzisha Mahakama Maalum kushughulikia wahalifu wanaojihusisha na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya. Maoni hayo yanaungwa mkono na Katibu Tawala wa mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja, anayeiomba serikali kuwa na sheria kali za kukabiliana na tatizo hili ambalo sasa limeanza kutoa matawi.
"Tushughulikie tatizo hili kwa juhudi za pamoja. Kila mtu mahala alipo ajione kuwa anao wajibu wa kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na usafirishaji kuanzia serikali za vijiji, wilaya mikoa na serikali kuu kuona kuwa uingiaji wa dawa hizi nchini unakomeshwa," anasema.
Anashauri juhudi zitakazofanywa kudhibiti tatizo hili ziende sambamba na kuwepo kwa sheria itakayosaidia sera ama mipango kazi ambayo madhumuni yake ni kupunguza madhara ya matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana katika vituo vya kubadilisha tabia na malezi kwa waathirika.
"Kote nchini tuungane kumkabili adui huyu ambaye ni kikwazo kwa nchi nzima kwani hakuna mkoa ambao hauna waathirika wa dawa za kulevya. Tuwe kitu kimoja kushiriki kumng'oa adui huyu ambaye mashambulizi yake yanakuwa ni ya kasi na ambayo athari zake tayari zimewakuta vijana wa mitaani, shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu," anasema Mtunguja.
Anasema kwa kuwa utafiti mbalimbali unaofanyika unaonesha kuwa tatizo hili la utumiaji unga na bangi limeingia katika shule kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu ni hatari na hili ni janga kwa nchi hii.
Hata hivyo Waziri katika ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Bungeni, William Lukuvi alisema katika kikao cha Bunge cha Novemba 2014 kuwa serikali itawasilisha muswada wa sheria ambayo itaweza kudhibiti tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na usafirishaji katika kikao kinachofuata, Januari 2015.
Muswada huo ambao tayari umesomwa kwa mara ya kwanza unatokana na hali halisi ambapo serikali na wadau wake wote imeamua kufanya marekebisho ya sheria hiyo Namba 9 ya mwaka 1995 baada ya kugundua kuwa yapo mapungufu makubwa. Alisema pamoja na ukweli kuwa kitengo cha Udhibiti Dawa za Kulevya Nchini chini ya kiongozi wake ASCP Geofrey Nzowa kinafanya kazi nzuri, mapungufu ya sheria hii huwafanya watuhumiwa wanaokamatwa mara nyingi kuachiwa.
Alifafanua kwa kueleza kuwa sheria hiyo Namba 9 ya mwaka 1995, inatoa mwanya kwa hakimu na hata jaji kuamua aina ya hukumu kwa mtuhumiwa anayetiwa hatiani.
"Sheria hii ya sasa inampa uwezo Hakimu ama Jaji kutoa hukumu ya ama kumpeleka gerezani au kulipa faini ama vyote viwili. Kwa sheria hii mpya mambo hayatakuwa hivyo, tunataka kuondokana kabisa na hali kama hii na badala yake sheria itaeleza wazi aina ya adhabu mtuhumiwa wa dawa za kulevya atapaswa kupewa," Lukuvi alisema.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuhakikisha kuwa wanatoa maoni yao kwa njia mbalimbali ili kuboresha kwa kuhakikisha kuwa Tanzania itaweza kudhibiti tatizo la matumizi ya dawa za kulevya kwa nguvu ya sheria ambayo itatoa uwezo kwa wahusika wote wanaopambana na tatizo hili.
Katika ushauri wake, Mntambo, mkulima na mwalimu anasema kuwa sheria hiyo itakapofika bungeni, sheria hiyo ihakikishe kuwa ina vipengele vyote muhimu na hatua kali dhidi ya wote wanaohusika na dawa za kulevya.
Anasema mambo ya kuzingatiwa katika sheria hiyo pamoja na kuziba mwanya kwa mahakimu na majaji katika kutoa adhabu ndogo ndogo ya kifungo ama ama faini, sheria izingatie pia katika kupiga vita kilimo cha aina yoyote cha mimea ya dawa za kulevya na uuzaji wake hasa bangi.
Anasema pia kuwa sheria hiyo mpya pia itoe mapendekezo ambayo yatamfanya mkulima kuwa na njia mbadala ya kuwa na kilimo cha mazao na kwamba mkazo uwekwe katika kilimo bora cha mazao makuu yanayoingiza fedha kwa taifa.
Anasema sheria hiyo itakuwa ni msaada mkubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya na usafirishaji, hasa katika kitengo cha udhibiti wa dawa za kulevya kama sheria itaweka kipengele cha kitengo hicho kupatiwa nyenzo za kisasa katika kutambua dawa za kulevya zinazofichwa kwa njia ya kutotambulika.
Pia anapendekeza kitengo kiwe na uwezo wa kutaifisha mali au bidhaa za watuhumiwa hao inapogundulika kuwa utajiri wao unatokana na dawa za kulevya.
Anasema, kama sheria hiyo ikipita kwa lengo la serikali na wadau wake katika kuwashughulikia watuhumiwa wa dawa za kulevya, anaamini kuwa Tanzania itarejesha sifa yake ya kuwa Bandari Salama. Lakini anashauri wananchi wengi zaidi kuwapa maoni wabunge wao kuhusu namna nzuri ya kuboresha sheria hiyo ili isaidie katika kumaliza tatizo la dawa za kulevya.
Kassim Mbegha ni mwandishi mkongwe wa habari nchini na mchangiaji katika gazeti hili.

HABARI LEO

Comments