Shinikizo dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, limezidi kupamba moto, baada ya idadi ya makundi ya kijamii yanayomuomba Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha kuzidi kuongezeka, ikiwa ni wiki tu moja tangu viongozi wa madhehebu ya Kikristo nchini kumtaka achukue hatua hiyo.
Hilo linatokana na Profesa Muhongo kuhusishwa katika kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Powere Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Safari hii Chama cha siasa cha ACT-Tanzania kimeungana na makundi hayo baada ya Mwenyekiti wake Taifa, Kadawi Limbu, kumuomba Rais Kikwete achukue hatua hiyo, ili kuvipa nguvu vyombo vya uchunguzi kufanya kazi yao.
Limbu, ambaye alizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, alisema tamko hilo ni sehemu ya maamuzi yaliyofikiwa na kamati kuu ya chama hicho iliyokutana jijini Dar es Salaam jana.
Alisema Rais Kikwete anapaswa kuchukua hatua hiyo dhidi ya Profesa Muhongo kwa kuwa Watanzania wanakabiliwa na maumivu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa dawa hospitalini, huku wengine wakiendelea 'kula raha' mitaani kwa fedha za wizi.
Limbu alisema hakuna ubishi kuwa fedha zilizokuwa zikihifadhiwa katika akaunti hiyo, zilikuwa ni za umma, kwani Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wizara ya Nishati na Madini, ambao ni wahusika wakuu katika suala hilo, ni taasisi za umma.
Alisema baada ya kashfa hiyo kubainika, Rais Kikwete alipaswa aanze kumshughulikia aliyehusishwa na vitendo vya udalali vilitengeneza mazingira yaliyotoa mwanya baadhi ya watu kuchota fedha hizo kifisadi kutoka katika akaunti hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema haoni mantiki kwa Rais Kikwete kumwajibisha aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na kumwacha kiporo Prof. Muhongo.
"Alipaswa aanze na aliyefanya udalali, vipi amweke kiporo? Rais Kikwete aone umuhimu wa Watanzania na maisha, akianza na hili atavipa nguvu vyombo vingine," alisema Limbu.
Alisema uwapo Rais Kikwete hatamwajibisha Profesa Muhongo, wabunge watakuwa na kila sababu ya kupiga kura katika mkutano wa Bunge ujao ya kutokuwa na imani waziri mkuu, ambaye ni kiongozi mkuu wa shughuli za serikali bungeni.
Desemba 25, mwaka huu, wakitoa salamu za sikukuu ya Krismas, viongozi wa madhehebu ya Kikristo nchini kwa nyakati tofauti, walimtaka Rais Kikwete kutowaonea haya viongozi wasiokuwa waadilifu wanaokwenda kinyume cha maadili katika kushughulikia mambo mbalimbali, kama vile fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo, badala yake achukue hatua za haraka kuwawajibisha na washitakiwe bila kusubiri kelele za wananchi.
Pia waliwataka watu waliohusika kwenye vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na kupokea mabilioni ya shilingi, kwenda kanisani kutubu badala ya kuzunguka huku na kule wakikanusha.
CHANZO: NIPASHE
Comments
Post a Comment