WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara MaalumU, Profesa Mark Mwandosya ameweka kiporo tangazo la nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao, aliposema, "sitatangaza nia, kwa sababu hapa si mahala pake."
Profesa Mwandosya ambaye katika kinyang'anyiro cha kupata mgombea urais wa CCM mwaka 2005, aliingia tatu bora na kushindwa na Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo juzi jioni jijini Mwanza, alipokuwa akihutubia katika Mahafali ya Chuo Kikuu cha St Augustine (SAUT).
Baada ya kuweka wazi kuwa hapakuwa mahali sahihi kwa yeye kutangaza nia, Profesa Mwandosya, aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika mahafali hayo, aliendeleza hotuba zake za kutoa mbinu mbalimbali kwa vijana wasomi, kuhusu namna bora ya kupata ajira katika soko la ndani na la kimataifa.
Waziri huyo aliwataka wasomi kuchagua fani zinazoajirika kirahisi, huku akiwaasa kuondoa woga na kuhisi kushindwa, wanaposhindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi kutokana na ubora wa elimu unaotolewa na vyuo vingi vya hapa nchini.
Alisema mwelekeo wa dunia ya sasa umeegemea zaidi katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, hivyo wanafunzi wanaohitimu katika maeneo hayo wanageuka lulu katika soko la ajira na hivyo kunufaika na elimu yao.
Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, pamoja na lugha ya Kiswahili kuwa lugha muhimu na adimu, bado wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kujenga umahiri katika kufahamu na kutumia lugha nyingine kama Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kichina, na hivyo kupata ajira katika sekta za umma, binafsi na nyinginezo kirahisi zaidi.
"Elimu mnayoipata hapa ni ya Kitaifa na si ya Kimwanza, kwa hiyo msijiwekee wigo wa kutafuta kazi za kitaifa na za kimataifa kwa kuzingatia ujuzi na maarifa mliyoyapata vyuoni," alisema Profesa Mwandosya.
Profesa Mwandosya pia alitaka wahitimu kuandaa akili katika kujiajiri wenyewe baada ya kuhitimu mafunzo, kutochagua kazi na kuweka malengo ya mbali zaidi badala ya kuweka malengo ya muda mfupi ambayo yanachangia mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Alijivunia hatua ya wanafunzi wengi aliowafundisha kujiajiri kwa kufungua kampuni zao binafsi, zinazofanya vizuri katika ushindani wa soko la ndani na nje ya nchi na kwamba hatua hiyo inampa faraja kubwa katika miaka 40 tangu alipopata Shahada yake ya Kwanza nchini Uingereza.
Mwishoni mwa Juni mwaka huu akiwa bungeni, Profesa Mwandosya alitoa ushauri kama huo kwa vijana wanaotafuta ajira, ili usaidie katika kukabiliana na kile wanasiasa wanachoita ajira ni bomu.
Aliwataka vijana wanaojiunga na vyuo vikuu, kuchukua kozi za sayansi na teknolojia na kuziunganisha na kozi za usimamizi wa biashara. Pia aliwataka kujifunza na kuelewa vema lugha ya Kiswahili na Kiingereza na angalau lugha nyingine kati ya Kifaransa ama Kihispania.
Pia alisisitiza umuhimu wa vijana kubuni mbinu za kujiajiri, kutochagua ngazi ya kuanzia, kuwa wabunifu na kujifunza kujiunga katika vikundi ili kupata mikopo.
HABARI LEO.
Comments
Post a Comment