Huku yeye akisema kuwa waraka wao una lugha ya UKAWA, wao wamesisitiza kwamba ni waraka wa kinabii, kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi.
Wakati yeye akikemea waraka wao, maaskofu wamesema ile ilikuwa sauti kutoka mbinguni, na kwamba anapambana na Mungu.
Wakati yeye akisema waraka wao haukuwa na utukufu wowote, wao wamemfananisha yeye na Goliati wa kwenye Biblia aliyeshindwa na Daudi kwa sababu ya jeuri na matusi kwa Mungu. Wamesisitiza kwamba kwa sababu ya jeuri yake, wataanzia pale atakapoishia baada ya Bunge Maalumu la Katiba.
Juzi na jana asubuhi, Sitta alitoa maneno ya kejeli dhidi ya viongozi wa Kikristo, hasa Jukwaa la Wakristo, ambao walitoa waraka kuonyesha kutoridhishwa kwao na mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba.
Sitta alitoa kauli hiyo bungeni alipokuwa akielezea mwenendo wa upigaji kura za kupitisha ibara na sura za rasimu ya katiba inayopendekezwa, akisema amekuwa akituhumiwa kwenye mitandao kwamba anadharau maaskofu.

Comments
Post a Comment