WAZIRI wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdalla Shaaban amesema Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi, ndiyo itakayotoa fursa kwa Zanzibar kuchimba mafuta na gesi, ambayo yameondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Amesisitiza kuwa ardhi ya Zanzibar haijauzwa na itatumika kwa maslahi ya Wazanzibari, kwa kadri itakavyoamuliwa na Baraza la Wawakilishi.
Shaaban alisema hayo katika mkutano wa hadhara wa wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika viwanja vya Demokrasia.
Alikuwa akifafanua baadhi ya kauli, ambazo zimekuwa zikitolewa na watu mbalimbali wanaopinga Katiba Inayopendekezwa.
Alisema Kifungu cha 23 na Kifungu cha 26 katika Katiba Inayopendekezwa, kimetoa nafasi kubwa kwa Zanzibar kuchimba rasilimali ya mafuta na gesi, jambo ambalo lilikuwa moja ya kilio kikubwa cha Wazanzibari kwa muda mrefu.
Alisema Kifungu cha 23 cha katiba hiyo, kinatamka wazi kwamba sheria zote za ardhi na mambo yake zitatungwa na Baraza la Wawakilishi.
"Mimi ndiyo msimamizi wa ardhi yote, si kweli kwamba mafuta hayataweza kuchimbwa kwa sababu ardhi ipo chini ya Muungano," alisema.
Alisema katika Kifungu cha 26, kinamtaka bayana kwamba rasilimali ya mafuta na gesi, sio mambo ya Muungano tena, ambapo Zanzibar itakuwa na uwezo wa kushughulikia nishati hiyo katika suala hilo.
"Kwa ufupi Katiba Inayopendekezwa, ndiyo mkombozi kwa wananchi wa Zanzibar ambayo imeweka mbele maslahi ya wananchi wake," alisema.
HABARI LEO.
Comments
Post a Comment