TUMESHASIKIA mengi kuhusu Mahakama ya Kadhi. Tumesikia bungeni, tumesikia katika vyombo vya habari na katika ripoti iliyotolewa na mwongozo kuhusu Mahakama ya Kadhi wakati wa utafiti wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2006.
Mjadala mzima ulianza Januari 1999, miaka 10 iliyopita wakati wa Sikukuu ya Idd el Fitr. Ni wakati huu ndiyo Waislamu walimuomba aliyekuwa mgeni rasmi, Rais mstaafu Benjamin Mkapa kusaidia kurejeshwa kwa mahakama hiyo.
Suala hili lilipelekwa bungeni na Thomas Ngawaiya kama hoja binafsi mwaka 2002. Kwa akili za watu wa kawaida ambao hawajalelewa na kuelewa misingi ya dini ya Kiislamu, kinachoingia akilini mwao ni nchi inataka kutawaliwa kwa “Sharia”, yaani sheria za Kiislamu ambazo hutumiwa kama mwongozo wa maisha ya kila siku katika nchi za Kiislamu.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Sura ya Kwanza, Ibara ya Tatu, Kifungu cha 19 inasema: “Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”
Sasa katika hili la serikali kushiriki katika mchakato wa kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi, ninaona kuwa, imekubali kufanya mabadiliko ya katiba bila kuwaambia wananchi, na kama haibadili katiba, basi haitafuata katiba na kama haifuati katiba, basi inapaswa kuondoka madarakani haraka, vinginevyo iseme kwa unyoofu bila kigugumizi kuwa, suala la Mahakama ya Kadhi liliingizwa kwa bahati mbaya katika ilani ya chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Iseme wazi kuwa kuendelea kujadiliwa kwake ni kuvuta muda au ‘danganya toto’, maana kamwe hatutegemei siku moja serikali ikatoa jibu ambalo litakwenda sambamba na kifungu cha katiba nilichokitaja hapo juu.
Akihutubia katika Chuo Kikuu cha Boston, Marekani, Septemba 25, 2006 kuhusu namna utawala wa kidemokrasia unavyofanya kazi ndani ya nchi yenye dini nyingi, mfano Tanzania, Rais Jakaya Kikwete alisema: “Suala la kutenganisha dini na siasa linatazamwa kwa umakini mkubwa ili kutoiingiza dini katika siasa wala siasa katika dini. Kutenganisha mambo hayo kunatiliwa mkazo sana.”
Hii ina maana kuwa, nchi yetu kikatiba haijihusishi na masuala ya kidini au kiroho na inazingatia uhalisia kuwa masula ya dini yanabaki kuwa binafsi kwa taasisi husika na kamwe serikali haitajihusisha na mambo hayo wala ya kiroho.
Katika nchi zinazotawaliwa kwa sheria za dini ya Kiislamu, kadhi huteuliwa na kiongozi wa nchi. Hata hivyo, katika nchi ambazo si za Kiislamu kama Tanzania, viongozi wa dini ya Kiislamu huchagua jina na kumpa rais kwa ajili ya kulitamka.
Mfano mzuri ni kama tulivyoona Rais Amani Abeid Karume akimwapisha Kadhi wa Zanzibar.
Baada ya uteuzi wa Kadhi na kuapishwa kwake, kazi inayofuata ni kwa kiongozi huyo wa kidini kuwateua wengine katika ngazi za mikoa na wilaya kadiri mfumo wa serikali wa kiutawala ulivyo. Hivyo kunakuwa na mahakama za wilaya, mkoa na rufaa.
Katika Mahakama ya Rufaa, hata Jaji Mkristo anaruhusiwa kuendesha mashtaka ila kwa masharti kuwa anapaswa kusaidiwa na masheikh wanne, au ulamaa (wasomi wazuri wa dini ya Kiislamu) na hukumu hufikiwa kwa kupiga kura ambapo uamuzi unatokana na kura zilizoshinda (simple majority).
Kazi ama wajibu wa kadhi katika Tanzania ni kutatua masuala yanahohusu ndoa, talaka na mambo yote hayo lazima yawahusu Waislamu wenyewe, wala si Muislamu na mtu wa dini nyingine, kwamba maamuzi kati ya Muislamu na mtu wa dini nyingine, lazima yaamuliwe na mahakama ya kiraia isiyoegemea upande wa dini yoyote.
Mahakama za kadhi zilizowahi kutajwa mahali kwingine duniani zinaweza kuwa mfano katika kuangalia je inawezekana na kwetu tukawa na kitu hiki?
Mahakama ya Kadhi, wazo mpaka lilipofika ni zuri ila serikali iache kupoteza muda wa Waislamu kushiriki katika tume kuunda mahakama hiyo. Waislamu kupitia Baraza la Ulamaa ndio wahusike zaidi kuliweka jambo hili katika mfumo wa utawala wa misikiti yao.
Serikali kuendelea kuwaahidi Waislamu juu ya suala hili binafsi naona kama danganya toto kwani itafika wakati litakuwa gumu kabisa katika utekelezaji. Je wakati huo itakuwa nani wa kulaumiwa, serikali au Waislamu?
Ikiwa kweli kwamba kadhi itabidi apendekezwe na Waislamu kisha aapishwe na rais, je tutakuwa na uhakika wa kuwa na Rais Mwislamu katika Tanzania siku zote? Na ikiwa siku moja tukawa na rais asiyeamini katika dini yoyote, je kadhi atakubali kuapishwa na mtu asiyesadiki uwepo wa Mungu?
Zaidi ya hayo, mambo ya kiroho yanaweza kuendeshwa kwa kufuata mifumo ya kiserikali? Mfano, kadhi akiamuru kuwa ndoa fulani ni batili, je ni lazima serikali itambue hili? Itakuwaje siku tukiwa na rais wa dini nyingine asiyesadiki katika imani hiyo?
Hofu yangu ni kuwa, jambo zuri kama hili la Mahakama ya Kadhi litakuja kuharibiwa endapo litakuwa na mchanganyiko na siasa za nchi. Mambo mazuri yanayopaswa kujadiliwa na Waislamu peke yao yatajadiliwa hata na wasio Waislamu.
Itafika wakati chombo hiki cha Mahakama ya Kadhi kitakosa heshima yake kama ambavyo imekuwa ikijitokeza siku hizi kwa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) kuonekana kama ni la kisiasa, hivyo kupingwa hata na baadhi ya Waislamu wenyewe.
Nionavyo mimi, kama kweli viongozi waliopo madarakani ni wakweli, watawaambia ukweli Waislamu kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi. Suala la kulinda heshima ya chama kwa kukubali hata mambo mazito yasiyowezekana kikatiba, ni udhaifu wa uongozi.
Waislamu wangependa suala la Mahakama ya Kadhi litambuliwe kikatiba, lakini serikali yenyewe iliyoapa kuilinda katiba, inapata ugumu kuamua maana kukubali huko ni kuipinga katiba iliyopo na kukataa ni kukiri kuwa iliwahadaa Waislamu.
Sitegemei hata siku moja kuwa serikali itasimama kidedea mbele ya Watanzania kuridhia mfumo wa Mahakama ya Kadhi ila ninachojua kwa sasa itafanya ujanja wa kuchelewa kutoa majibu ili hatimaye ifike wakati wa uchaguzi mkuu.
Waislamu waunde mahakama yao ya kadhi watakayokuwa na uhuru wa kufanya kazi bila vurugu za kisiasa, watakuwa huru kuamua kwa kuangalia mambo yao kwa mtazamo wa imani yao bila kuathiriwa na watu ambao si Waislamu. Mambo ya Waislamu yaamuliwe na Waislamu wenyewe, kutegemea serikali kutaendelea kuwanyima Waislamu fursa ya kutumia uhuru wao na hakutatatua matatizo mengi ambayo yamekuwa yakiwakumba kwa sababu tu wanashirikisha serikali kupata maamuzi yanayohusu dini yao.
Wajitegemee si katika hili tu, ila katika mambo mengi, mfano kuandaa safari za hija huko Makka. Waislamu wamekuwa wakisumbuka kusafiri kwenda Makka wakati wa hija kutokana na baadhi ya watu kutokujua umuhimu wake. Na hii ni kwa sababu wana itikadi tofauti za dini au hawaamini uwepo wa Mungu.
Tutaendelea kudumisha amani endapo kila kitu kitaamuliwa na wenye mamlaka ya kitu husika, tusitegemee maamuzi ya wakulima yaamuliwe na wafugaji na maamuzi ya wavuvi yaamuliwe na makandarasi, tutajichanganya.
Maamuzi ya kidini yasiamuliwe na wanasiasa, wengi wanaendelea kusadiki kuwa siasa ni mchezo mchafu, sasa itawezekanaje kilicho kichafu kitumike kutoa kilicho safi?
Mambo ya dini ni masafi, ni matakatifu na hayana upande wowote. Siasa zina upande na zinajihusisha zaidi na maslahi ya dunia, lakini mambo ya dini yanahusu miongozo ya Mungu.
Serikali kuendelea kusema tutawapa maamuzi kwa jambo hili nyeti la Mahakama ya Kadhi wakati linaonekana wazi haliendani na katiba iliyopo, ni ucheleweshaji wa makusudi ambao si wa muhimu kwa maendeleo ya Waislamu.
Serikali itaendelea kuvuta muda kwa malengo ya Uchaguzi badala ya kufikia maamuzi jambo ambalo inabidi lipate tafakari ya kina.
Comments
Post a Comment