Mrema azidi kubezwa jimboni kwake


NA GODFREY MUSHI
20th September 2014


Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema

Siku chache baada ya Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema kuhoji uhalali wa Mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia kupigiwa wimbo wa taifa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR-Mageuzi, Hemed Msabaha amesema Mrema 'anaweweseka' baada ya kugundua wapiga kura wake wamemgeuka kwa kitendo chake cha kuliunga mkono Bunge Maalum la Katiba kuendelea.

Mrema na Mbatia wameingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya mmoja kati yao kumshitaki mwenzake kwa Rais Jakaya Kikwete kwamba anatumia jina lake vibaya kumvuruga jimboni humo wakati muda wa kampeni za uchaguzi mkuu ujao bado haujatangazwa rasmi.

Msabaha aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa kuwa, Mrema amepoteza mwelekeo wa kisiasa na kujiondoa taratibu katika medani hiyo kwa kile alichokiita kulewa madaraka kwa kujisahau kwamba alipata ridhaa ya umma ya kuliongoza jimbo hilo kutoka kwa wananchi hao anaowabeza kwa kumwimbia Mbatia wimbo wa taifa.

Mgogoro huo umeibuka baada ya Mbatia kuwa kiongozi wa kwanza wa Ukawa kutangaza nia ya kugombea ubunge Vunjo na kuachana na dhamira ya kuwania nafasi ya urais kupitia chama chake cha NCCR-Mageuzi.

Wengine waliotangaza nia katika jimbo hilo ni pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri na Bunge wa Chadema,John Mrema na mwandishi binafsi wa zamani wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Afrika Mashariki,  Exaud Makyao.

Mbatia alisema ameitikia wito wa wananchi wa Vunjo waliomwomba aachane na dhamira yake ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na badala yake, kurudi nyumbani kwa lengo la kuyasikiliza matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi.

Alisema Mrema ameshindwa kubaini kwamba Mbatia ana uhuru wa kushiriki shughuli za umma katika eneo lolote la Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1984 namba 15, na ibara ya 6 ya sheria ya mwaka 1999 namba 34 ibara ya 4 akiwa kama Mbunge wa Kuteuliwa na Rais (Jakaya Kikwete) katika nafasi 10 alizopewa kikatiba.
 

CHANZO: NIPASHE

Comments