ANNA MGHWIRA KWA KATIBU WA BAWACHA TAIFA NA SOFIA MWAKAGENDA KWA MWENYEKITI BAWACHA TAIFA


Wito umekuja kuwa wagombea wengine walio ndani ya mabadiliko nao walete wasifa na majina yao jukwaani - shukurani Nanyaro kwa kuanzisha. 

Mimi Anna Elisha Mghwira - pia nimeonyesha nia kushika wadhifa wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia - CHADEMA - katika Baraza la Wanawake. Ninawania nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Bawacha Taifa. 

Wanawake ni Jeshi Kubwa, na kama ilivyo kwa kila jeshi lazima kuwa na Kamanda / Jemadari kuliongoza. Wakati umefika wa kutafuta viongozi kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo na mimi Anna na dada Sofia tumeonyesha nia zetu katika mchakato huu. 

Sofia ataendeleza zaidi wasifa wake. Natoa wa kwangu hapa. 

Kwanza tushukuru kupewa kuuona tena mwaka huu na kipindi hiki cha mwisho wa mwaka wa uchaguzi ndani ya Chama. Tuchaguane kwa amani na nia ya kujenga. 

Kama mgombea nafasi ya uongozi wa wanawake, sifa yangu kuu ya kwanza ni kwamba mimi pia ni mwanamke. Ya pili ni mwanamke anayependa maendeleo yake mwenyewe na ya wanawake na wanaume pia ili kulea usawa wa uumbaji aliotupa Mungu mwenyewe - usawa wa majukumu na fursa. 

Nimepata fursa ya kupata elimu ya shule licha ya elimu ya jamii iliyonilea ya Warimi / Wanyaturu wa Singida - wazazi wangu wote wakitokea iliyo sasa manispaa ya singida: Kule shule nilisoma kusoma na kuandika na hesabu, baadae theologia ya Kizungu ambayo nimejaribu sana kuipa maana kama mwanamke wa Kiafrika. Pia nikaongeza kidogo sheria za kizungu na Khindi kwa sababu za ukoloni. Na kwa undani nikaongeza sheria za Kimatiafa za Haki za Binadamu. Hizi nazo najaribu kuzipa maana katika maisha mapana ya mwanamke wa Kiafrika Mtanzania. 

Ndani ya Chadema ninachanganya na kushiriki  majukumu kati ya Kanda ya kaskazini na Kanda ya kati, kwa sababu ninaishi na kufanya kazi kanda ya kaskazini na ninajiandaa kuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini. Majkumu yangu ni pamoja na:

1. Nilikuwa Mwenyekiti wa Bawacha Arumeru / sasa ni Katibu Bawacha Mkoa / Mhe Rebeka Mngodo (MB) ni Mwenyekiti mpya Arumeru bada ya uchaguzi huu. 

2. Mshauri wa vijana na wanafunzi

3. Mjumbe Kamati ya Kanda ya kati / nimeshiriki pia vikao vya Kanda ya Kaskazini kwa nykati tofauti. 

Hali ya kuchanganya kanda na majimbo (niligombea pia Arumeru Mashariki ninakoishi) imenipa kukijua vema chama: nguvu, udhaifu, fursa na changamoto za maeneo na maendeleo kichama na kitaifa. . 

Uzoefu huu umenipa wito wa kusogea mbele kushika wadhifa wa Kitaifa ambako kanda zote hukutana. Ninaamini fursa hii itanipa wigo mpana wa kukijua na kujua njia bora za kukitumikia chama na watanzania kwa ujumla wake. 

Niseme pia kuwa utendaji wangu umetengeneza hali ya kuhitajiwa ( created demand for service) nje ya mipaka ya nafasi rasmi kichama na Kijamii. Wanawake wa kada na itikadi zote - wengi hasa wa ninakotoka na ninakoishi wameonesha imani hii kwa mambo mbalimbali ya maisha, kazi, furaha na huzuni. 

Ninamuomba Mungu na Wanawake wa CHADEMA waridhie kunipa nafasi ya Ukatibu tufanye kazi kwa pamoja kuwainua wanawake wa Tanzania kwa hatua nyingine mbele tokea pale walipoishia waliotutangulia. 

Kwa heshima na unyenyekevu niweke katika ukiurasa wa jukwaa hili. 

Madam spika - njiwa mwenye makinda

Comments