Uraia pacha utaendeleza ufisadi
Uraia pacha utafanya watu wa nje matajiri wanunue ardhi yetu yote
Uraia pacha ni kukosa uzalendo
Uraia pacha na ufisadi
Hivi hili ni la kweli? Je, tunataka kusema wale Watanzania wenzetu walioko diaspora wote ni mafisadi na hiyo ndio sababu ya wao kutaka uraia pacha? Na kweli wao ni mafisadi zaidi ya hawa mafisadi tulio nao humu nchini? Na hawa mafisadi tuliojaza nchini ni raia pacha wa nchi gani? Na ni ufisadi gani ambao mtu akiwa raia pacha ataufanya - kuondoka na shilingi ya Tanzania kupeleka nje? Kutorosha nyara za serikali? Au kuleta fedha za kigeni nchini? Hata kama ni kutorosha nyara na fedha, sheria na kudhibidi hayo mambo, kama money laundering laws, zitakuwa wapi?
Uraia pacha utafanya matajiri wa nje wanunue ardhi yetu yote
Kwani nani aliyesema tukiruhusu uraia pacha ina maana kila mtu aliyeko nje anaruhusiwa kuwa raia wa Tanzania na kuwa raia pacha akiomba uraia wetu? Hii inaonekana kuwa watu hawajui kwamba walengwa wa kwanza wa uraia pacha ni Watanzania ambao wako nje, ambao wengi wao wanaogopa kuchukua uraia wa huko nje wakihofia kupoteza uraia wa Tanzania, kulingana na sheria ya sasa ya uraia. Na walengwa wa pili ni raia wa nje ambao labda wameoa au kuolewa na Watanzania, na wangependa kutambulika kama raia wa Tanzania pia. Na mwisho ni raia wa nje waliokaa sana nchini na kupata ukazi wa kudumu akini bado wana uraia wa kwao. Sasa hili la matajiri kuchukua ardhi yetu linatoka wapi? Na hata kama ukioa au kuoelewa, kuna sheria ambazo hazikuruhusu kuwa raia wa Tanzania mara tu ukioa bali hadi miaka kadhaa ipite ukiwa mkazi wa hapa nchini. Sasa tatizo liko wapi?
Uraia pacha ni kukosa uzalendo
Jamani, hebu tachane na hizi kauli za kipropaganda. Kwani uzalendo maana yake nini au unaonyeshwa kwa vitendo gani kiasi kwamba mwenye uraia pacha aone kuwa na uzalendo pungufu ya yule asiye na uraia pacha? Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba wanaotaka uraia pacha wana hiyo ari kwa ajili ya uzalendo walio nao na Tanzania. Japo wameishi nje muda mrefu bado wanaona shida kukata mizizi na nchi yao Tanzania. Angalia kwamba nchi kama Norway na Israel zina raia wengi nje ya nchi kuliko wale walio ndani ya nchi; na hawa walioko nje uzalendo wao haujapungua hata kidogo kwa kuwa tu wamekuwa raia wa huko wanakoishi. Juzi hapa nimesikia Mkurdishi wa Iraq, yeye na mwanae, ambao kwa sasa ni raia wa Sweden, wamerudi Iraq kwenda kupigana dhidi ya ISIS. Sasa anayesema uraia pacha ni kukosa uzalendo, ni kwa kigezo kipi?
Comments
Post a Comment