RAIS Jakaya Kikwete amesema yupo tayari kukutana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili kunusuru mchakato wa Katiba mpya.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kupinga hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumtuma Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, kusaka suluhu na viongozi wa Ukawa.
Akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro juzi, mara baada ya kusoma risala yao na kuunga mkono Bunge la Katiba, Rais Kikwete alisema hana
sababu ya kutokutana na viongozi waliosusia vikao vya Bunge.
Alisema kutokana na hali hiyo, yupo tayari kukutana nao, na kwamba wanajua namna ya kukutana naye ili waweze kufanya mazungumzo yatakayoliwezesha taifa kupata Katiba mpya.
"Mimi sina tatizo la kukutana nao. Wanajua jinsi ya kukutana nami ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi.
"Mimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri. Mchakato ni mgumu, lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria kweli kweli tutafika tuendako vizuri," alisema Rais Kikwete.
Alisema anasikitishwa na tofauti za viongozi wa siasa na kuleta mfarakano kwa taifa, hali ya kuwa tangu awali aliwaambia kuwa wakijiruhusu kushindana na kuviziana ni wazi mchakato wa Katiba utakwama.

Comments
Post a Comment