Jeshi la Polisi laanza Uchunguzi wa tukio la Basi la Magereza lililokuwa limebeba Wafungwa kushambuliwa kwa Risasi
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, wanafanya uchunguzi wa tukio la kushambulia basi la Magereza lenye namba za usajili T 0046, aina ya Isuzu, Julai 2 mwaka huu, eneo la Mikocheni, karibu na Regency Hotel, Kata ya Msasani, Wilaya ya Kipolisi Oysterbay, Mkoa wa Kinondoni.
Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea saa 7:30 mchana ambapo watu wawili wasiofahamika waliokuwa wakitembea kwa miguu, walilishambulia basi hilo lililokuwa likiendeshwa na askari mwenye namba A.9716 SGT Musofe.
Alisema basi hilo lilikuwa na mahabusu 15 likitokea katika Mahakama ya Mwanzo Kawe kwenda Gereza la Segerea, wakisindikizwa na askari Magereza pamoja na polisi kwa wakati mmoja.
"Wakiwa kwenye foleni, ghaflawalitokea watu wawili waliokuwa wakitembea kwa miguu wakielekea lilipo basi hili, mmoja kati ya watu hao alianza kufyatua risasi akizielekeza kwenye basi.
"Tukio hili lilisababisha kuvunjika kwa kioo cha mbele, nyuma na ubavuni, askari watatu walijeruhiwa akiwemo SGT Musofe aliyekuwa dereva ambaye alipata majeraha mkono wa kulia, askari wa kike WP. 4481 CPL Dotto (33), mkazi wa Tegeta Kanisani, alijeruhiwa titi la upande wa kushoto na kulazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili," alisema.
Aliongeza kuwa, hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri ambapo mahabusu Doreen Damian (19) alijeruhiwa lakini alitibiwa na kuruhusiwa.
Wakati huo huo, Kamishna Kova alisema jeshi hilo linamshikilia jambazi sugu Hassuan Mohamed kwa jina maarufu Mudo (28), mkazi wa Tandika aliyekuwa akifanya matukio ya uhalifu kwa kutumia silaha.
"Jambazi huyu tulimuwekea mtego wakati yeye na wenzake wawili wakijiandaa kufanya tukio la ujambazi jijini...alikamatwa Julai 2 mwaka huu, eneo la Tandika muda mfupi kabla ya hawajakamilisha uporaji." Alisema Kova
Alisema bunduki hiyo ambayo imefutwa namba zake za usajili, ilikuwa ya magazine yenye risasi 27 ambapo juhudi zinaendelea ili kuwanasa majambazi wengine wanaounda mtandao huo ambao walikimbia

Comments
Post a Comment